
Vyama
vya Siasa 21 vinavyotarajiwa kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa Rais,
wabunge na Madiwani baadaye mwaka huu vimesaini Maadili ya uchaguzi
yatakayotumika wakati wa kampeni, kupiga kura na wakati wa kutangaza
matokeo.
Maadili
hayo yanayohusisha Serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Vyama
vya Siasa yalisainiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dr. Florence
Turuka, Mwenyekiti wa NEC Jaji Damian Lubuva na Wawakilishi wa vyama vya
Siasa 21 nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume
hiyo amesema Chama cha Wananchi (CUF) hakikusaini Maadili hayo kutokana
na kuwa na kazi nyingine lakini akasisitiza kuwa Chama hicho kitasaini
Maadili hayo wakati wowote.
Akifafanua
kuhusu Maadili hayo, Jaji Lubuva alisema Maadili yanapaswa kuanza
kutumika rasmi Agosti 22 mwaka huu wakati kampeni za uchaguzi
zitakapoanza, katika kipindi cha kupiga kura na wakati wa kutangazwa kwa
matokeo ya uchaguzi huo.
Alisema
Maadili hayo pia yatahusu wajibu wa vyama vya siasa na wagombea na
mambo yasiyotakiwa kufanywa na vyama vya siasa na wagombea.
Maadili
pia yatahusu masuala yanayotakiwa kufanywa na yasiyotakiwa kufanywa
wakati wa kupiga kura.Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa maadili
yaliyosainiwa pia yatahusu maadili kwa Tume ya Uchaguzi yaani mambo
yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanywa na Tume hiyo.


0 comments :
Post a Comment