CCM imeshatangaza kuwa itatumia vigezo 13 ilivyojiwekea kuwachambua
wagombea 41 waliochukua na kurejesha fomu ili kupata majina ya wachache
watakaopigiwa kura na mkutano huo mkuu, lakini Kamati ya Wazee, ambayo
itatoa ushauri utakaokuwa msingi wa uamuzi wa vikao vingine na Kamati
Kuu, italazimika kuangalia sifa za ziada katika kuchuja watangazania
hao.
Kamati ya Wazee, inayohusisha wenyeviti na makamu wao wa zamani wa CCM
pamoja na marais wa zamani wa Zanzibar, imeripotiwa kuanza kazi ya
uchambuzi na itawasilisha taarifa yake kwa Kamati Kuu itakayokutana
Julai 9 na baadaye kupeleka mapendekezo yake kwenye Halmashauri Kuu,
ambayo huandaa ajenda za Mkutano Mkuu.
Wakati vikao hivyo vikiandaliwa, uzoefu unaonyesha kuwa CCM huzingatia
mambo mengi katika kufanya uchambuzi, ikiwa ni pamoja na uteuzi wa mtu
atakayeondoa makundi yaliyoundwa wakati wa kuelekea uteuzi wa mgombea
urais wake, kuzingatia Muungano, jinsia, eneo la kijiografia, rekodi ya
mtiania, mustakabali wa uongozi wa chama na kukubalika kwa kada, hasa
katika kipindi hiki ambacho upinzani umeongezeka nguvu.
“Kuna katiba za aina mbili,” alisema mmoja wa makada ambaye aliomba jina
lake lisitiriwe. “Katiba ya maandishi ambayo inatoa mwongozo wa
kisheria wa namna ya kumpata Rais wa nchi, lakini pia kuna katiba ya
kimtazamo ambayo si rasmi, bali ni fikra za watu wanapozungumzia aina ya
rais wanayemfikiria.
“Mfano, kama kuna eneo fulani halijawahi kutoa kiongozi wa nchi, kipindi hiki sasa ni chao.”
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi uliojumuisha mahojiano
na baadhi ya makada wenye uzoefu na mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM,
mgombea wa chama hicho tawala anaweza kutoka katika makundi manne ambayo
gazeti hilo limeyaita kundi la kifo, kundi la mteule mbadala, kundi la
vijana na wanawake.
Iwapo mteule hataweza kutoka kwenye kundi la kifo, ambalo linajumuisha
makada wenye nafasi kubwa ya kupitishwa, chama hicho kinaweza kuamua
kuchukua mwanachama ambaye atatoka kundi la wateule mbadala kwa lengo la
kuzika makundi makubwa yaliyozuka wakati huu, au kuteua kada kijana
iwapo CCM itakuwa inataka mwelekeo mpya, au mgombea mwanamke kama
ilivyokuwa mwaka 2010 ilipoamua kuachana ghafla na Samuel Sitta na
kumweka mbele Anne Makinda kuwa Spika wa Bunge, kwa maelezo kuwa umefika
wakati wa wanawake.
Kundi la kifo
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, kundi la kifo linaweza kuwa na makada sita
ambao ni Profesa Mark Mwandosya, Steven Wasira, Frederick Sumaye,
Edward Lowassa, Bernard Membe na Mizengo Pinda.
Katika kundi hilo, Mwandosya amekuwa hahusishwi na kashfa wala kuwa na
migogoro na makada wengine. Aligombea kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na
kushika nafasi ya tatu, akiwa nyuma ya Jakaya Kikwete, aliyeshinda na Dk
Salim Ahmed Salim.
Pamoja na kutokuwa na mivutano na watu, Profesa amekuwa hasikiki kutokana na kupewa kazi inayomweka mbali na wananchi.
“Kuendelea kuwamo ndani ya Serikali hadi sasa, katika macho ya wengi,
ataonekana hana jipya,” alisema mchambuzi huyo akimzungumzia Profesa
Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu).
Kundi hilo pia linamjumuisha Wasira ambaye uzoefu wake mkubwa ndani ya
chama na Serikali unampa nafasi kubwa ya kupewa dhamana hiyo. Amekuwa
akitumiwa na CCM kutetea utendaji wa Serikali na hivi sasa amepewa
jukumu la kuongoza kamati inayoandaa Ilani ya Uchaguzi.
Ukweli ni kwamba anatoka Kanda ya Ziwa, ambayo kichama ni kubwa kwa
maana ya idadi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu, jambo linalompa nafasi kubwa
ya kushinda iwapo jina lake litakwenda kwenye chombo hicho cha mwisho
cha uamuzi.
Lakini nafasi yake inakuwa finyu kutokana na wakosoaji kumwona kuwa
amepoteza mvuto baada ya kufanya kazi kwenye Serikali za awamu zote nne
bila ya kuwa na kitu kinachomtofautisha na wengine na hilo linaweza
kuipa nguvu Kamati Kuu kumwengua.
Pia, wamo mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa
ambao wote walishawahi kuingia bila mafanikio kwenye mbio za urais kwa
tiketi ya CCM.
Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo katika
Serikali ya Awamu ya Tatu, aligombea mwaka 2005 lakini jina lake
lilikatwa. Ni mtu ambaye hana makundi kwenye chama, amepangua tuhuma
dhidi yake na daima amekuwa akionyesha wazi chuki yake dhidi ya rushwa.
Baada ya mawaziri wakuu kugonga mwamba katika chaguzi zilizopita, safari
hii Sumaye atakuwa akitegemea kuwa, kati ya watatu walio kwenye
kinyang’anyiro hicho, atapitishwa.
Lakini uzoefu wake kwenye nafasi ya waziri mkuu kwa kipindi chote cha
miaka 10 na chuki yake ya wazi dhidi ya rushwa, hakuwezi kuwa sifa
pekee. Bado hajajiimarisha ipasavyo ndani ya chama, ambacho kwa kumteua
mgombea urais, kitakuwa kimempata mwenyekiti wake wa miaka 10 ijayo.
Atalazimika kushinda ushawishi wa wapinzani wake waliowahi kushika nafasi hiyo, Lowassa na Pinda ili apitishwe na CCM.
Kamati Kuu itakuwa na kazi ngumu itakapokutana na jina la Lowassa,
Mbunge wa Monduli ambaye alikuwa amekaa kimya kwa muda mrefu tangu
alipojiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008 kutokana na sakata la Richmond,
lakini amerejea kwa kishindo katika miaka miwili iliyopita.
Lowassa amejijenga ndani ya CCM na ameonyesha nguvu yake ya kuungwa
mkono na wanachama na watu wengine walio nje na pia wakati alipotangaza
nia na baadaye kuzunguka mikoani kusaka wadhamini.
Kauli ya Rais Kikwete kuwa CCM inataka mtu ambaye anaungwa mkono ndani
na nje ya chama imeitia nguvu kambi yake na amekuwa akitumia kauli ya
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ya chama hicho kuongoza mabadiliko,
akijinadi kuwa ndiye anayeweza kuongoza mabadiliko hayo.
Mtaji wake wa wanachama, wabunge, wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mkutano
Mkuu ambao wamejitokeza bayana kuonyesha msimamo wao, ndiyo unaompa
nafasi kubwa.
Msuguano wa maneno kati yake na Katibu wa Uenezi, Nape Nnauye unaweza
kumpa nguvu ya kuituhumu Sekretarieti ya CCM kuwa inamfanyia njama, kama
mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru alivyoeleza kwenye
moja ya mikutano yake.
Hata hivyo, kundi lake limekuwa na msuguano na kundi la kada mwingine,
Bernard Membe, hali iliyokifanya chama kuonekana kimegawanyika makundi
mawili.
Pia, ingawa hakuna mtu anayeelekeza kwake tuhuma za moja kwa moja kuwa
anahusika kwenye ufisadi zaidi ya Kamati ya Bunge iliyomtaka ajitathmini
kuhusu kuhusika kwake kwenye sakata la Richmond, wapinzani wake
wamekuwa wakitumia mitandao ya jamii kumhusisha na kashfa
hiyo.Alilazimika kujibu tuhuma hizo siku ya kurudisha fomu alipotaka
wanaomtuhumu wajitokeze.
Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pia
anaingia kwenye kundi hili kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya
kujikubalisha ndani ya chama.
Tangu Benjamin Mkapa atoke kwenye wizara hiyo na kuwa Rais mwaka 1995 na
kufuatiwa na Kikwete, wizara hiyo inaonekana kuwa ni bomba la
kupitishia marais. Membe ameshikilia wizara hiyo kwa takriban miaka
minane. Mbunge huyo wa Mtama amekuwa hahusishwi na mambo machafu na
yanayokera wananchi.
“Huwezi kupitisha mtu ambaye ni kero kwa wananchi,” alisema mchambuzi mwingine kutoka ndani ya chama hicho.
Baada ya kuhusishwa kwenye mitandao ya kijamii na fedha kutoka Libya,
Membe aliamua kutoa ufafanuzi wa fedha hizo zinazokadiriwa kuwa Sh40
bilioni, akisema hakuzichota na kwamba maelekezo ya matumizi ya fedha
hizo yalitolewa na Mahakama.
Tatizo linalosumbua kwa mtiania huyo ni msuguano baina ya kambi yake na
ile ya Lowassa, ambao unaonekana kukigawa chama. Ufinyu wa nafasi yake
pia unatokana na kanda anayotoka kutokuwa na nguvu kubwa ndani ya chama.
Waziri Mkuu Pinda pia anaingia kwenye kundi hili kutokana na rekodi yake
ya kustahimili kushikilia nafasi hiyo kwa miaka minane tangu ateuliwe
mwaka 2008, kutokuwa na kashfa na pia kutokuwa na vitendo vinavyokera
wananchi.
Pinda, ambaye anajinadi kama “mtoto wa mkulima”, aligeuza mwelekeo wa
mbio za urais baada ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho na katika
kipindi kifupi kuonekana amepata wafuasi wengi. Ni mwadilifu na
ameonyesha nidhamu kwa chama wakati wote, hasa katika hotuba zake wakati
wa kusaka wadhamini, akieleza kuwa ataanzia pale ambako Rais Kikwete
ataishia.
Kundi la mteule mbadala
Kundi la pili linahusisha makada ambao wana nafasi ya kupitishwa na
kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, ikiwa ni mpango mbadala wa
kuzima makundi yaliyojitokeza kwenye mbio za urais, au kama Kamati Kuu
itaridhika kuwa makada hao sita wa kundi la kwanza wamepoteza sifa kwa
kuangalia vigezo tofauti.
Katika kundi hili, wapo Dk Mohamed Ghalib Bilal (ambaye ni Makamu wa
Rais), Jaji Augustino Ramadhani, Balozi Amina Salum Ali, Makongoro
Nyerere, Balozi Ali Karume, Dk John Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi
na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.
Dk Magufuli, ambaye ameingia kwa mara ya kwanza kwenye mbio za urais,
ndiye anayeweza kushangaza wengi iwapo atapitishwa na Kamati Kuu kwenda
kupigiwa kura. Rekodi ya utendaji wake ni bayana na karibu mawaziri 10
waliochukua fomu wametumia ujenzi wa miundombinu ya usafiri kuwa ni
mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne ambayo alihusika.
Dk Magufuli hana madoa ya ufisadi wala utendaji mbovu na daima amekuwa
akionyesha unyenyekevu kwa Rais Kikwete kila alipozungumzia mafanikio ya
wizara yake. Nguvu ya Kanda ya Ziwa ndani ya chama inamfanya awe na
nafasi kubwa ya kupitishwa kugombea urais iwapo jina lake litapelekwa
kwenye Mkutano Mkuu.
Ufinyu wa nafasi yake kuteuliwa ni pale Kamati Kuu itakapokata jina lake na kumweka mtu mwingine kutoka kanda yake.
Kundi hili pia lina jina jingine kubwa lililokuwa likizungumzwa sana
kabla ya mbio za urais kuanza, Jaji Ramadhani. Mwanasheria huyo mkuu wa
zamani ana sifa na fursa nyingi za kupenya kwenye mchujo. Moja ya sifa
zake kuu ni uadilifu, lakini pia ana Uzanzibari na Ubara ndani yake
unaomfanya aweze kukubalika na pande zote mbili, hasa Zanzibar ambayo
pia ina nguvu kubwa katika kufikia uamuzi.
Jaji Ramadhan pia ni tiba ya tatizo la makundi yaliyopo kwenye mbio za
urais. Lakini wakosoaji wameshaanza kuhoji uhai wa uanachama wake na
muda aliokuwa ndani ya CCM kutokana na ukweli kuwa amekuwa mtumishi wa
Serikali wa ngazi ya juu na hivyo hakutakiwa kujihusisha na siasa.
Anajitetea kuwa alihuisha uanachama wake miaka mitatu iliyopita baada ya
kustaafu. Suala la uanachama linahusisha pia nafasi yake ya kuwa
mwenyekiti wa CCM, nafasi inayokwenda sambamba na urais. Katika kundi
hili pia yupo, Dk Bilal ambaye anaingia kwenye kinyang’anyiro akiwa na
kete ya usafi, lakini pia Uzanzibari ambao kama utaibuka kwenye vikao
hivyo, makamu huyo wa rais, anaweza kuwa na nafasi kubwa.
Changamoto kwake ni kukubalika kwake ndani ya chama kama ilivyojionyesha
kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Zanzibar ambayo inaonyesha, licha ya
kukubalika kwenye vikao vya chama upande wa visiwani na kuongoza kwenye
kura ya maoni alipogombea urais wa Zanzibar, alishindwa kuwashawishi
wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma na kufanya jina lake
lishindwe na kuibuka la Amani Abeid Karume ambaye alikuwa mgombea wa CCM
Zanzibar na alishinda urais.
Suala la wanawake pia linajitokeza kwenye kundi hili, ambalo wamo Dk
Migiro na Balozi Amina. Wote wameliwakilisha Taifa kwenye Umoja wa
Mataifa, lakini Dk Migiro ndiye aliyepata umaarufu zaidi baada ya
kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chombo hicho na sasa ni mmoja wa
mawaziri waandamizi.
Jina lake linaweza kupenya kwenye tano bora na hatimaye kupitishwa na
CCM kuwania urais iwapo kundi la kwanza litaonekana halina mgombea
mwenye sifa kwa kuangalia vigezo tofauti. Changamoto kwa waziri huyo wa
zamani wa mambo ya nje ni nguvu yake ndani ya chama na uwezo wa
kustahimili mikiki mikiki iwapo atakuwa mwenyekiti.
Balozi Amina amefanya kazi kwa muda mrefu ubalozini na hivyo kupata
uzoefu mkubwa wa uongozi akiwa mwanadiplomasia. Hana madoa ya uchafu
wala kuwa kero kwa wananchi na nafasi yake ni pale tu suala la wanawake
na Uzanzibari litakapochukua nafasi.
Vilevile, Balozi Karume anaingia kwenye kundi hili akiwa moja ya tiba za
tatizo la makundi, lakini pia suala la Muungano linampa nafasi ya
ziada.
Butiama ilikuwa imesahaulika hadi zilipoibuka taarifa kwenye mitandao ya
kijamii kuwa Makongoro Nyerere anaandaliwa kumrithi Kikwete. Imani hiyo
iliimarika baada ya mtoto huyo wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu
Nyerere, kujitokeza.
Alitumia nafasi ya kutangaza nia kuwachambua watiania wenzake, akiwataja
baadhi kwa majina na udhaifu wao. Amefanya kazi kubwa ya kukumbusha
wanasiasa umuhimu wa falsafa za Baba wa Taifa na anaonekana kuwa na
nafasi ya kupitishwa iwapo ataingia tano bora, akiwa hana madoa zaidi ya
kuhama chama mwaka 1995 na kujiunga na NCCR, nguvu ya Kanda ya Ziwa na
ujasiri wa kukemea utovu wa nidhamu ndani ya CCM vinaweza kumbeba.
Kundi la Vijana
Kundi la vijana limeweka changamoto kubwa kwenye uchaguzi wa CCM mwaka
huu, likiongozwa na makada kama January Makamba, William Ngeleja, Dk
Mwele Malecela, Luhaga Mpina, Dk Hamisi Kigwangalla, Mwigulu Nchemba na
Lazaro Nyalandu na baadhi ambao si maarufu na wengine hawana sifa
zinazotakiwa kikatiba.
Nchemba ndiye anaongoza kwa kupewa nafasi katika kundi hili la vijana na
kuna uwezekano akaingia tano bora. Alijiuzulu nafasi ya Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Bara ili ajikite kwenye mbio hizo za urais.
Kwa kutumia nafasi yake, ameweza kujijenga ndani ya CCM huku misimamo
yake wakati wa sakata la escrow, Bunge la Katiba na udhibiti wa matumizi
ya Serikali vikimpatia umaarufu ndani ya chama hicho.
Pia, yupo January Makamba ambaye amekuwa mwandishi wa hotuba wa Rais
kabla ya kugombea ubunge wa Jimbo la Bumbuli na baadaye kuteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Makamba ameeleza bayana kuwa CCM inahitaji fikra mpya na hivyo kutakiwa
kuongozwa na kijana ambaye atafanya mageuzi. Lakini alianza kukosolewa
mara tu alipotangaza nia, huku Rais Kikwete akieleza kushtushwa na
taarifa hizo. Dk Kigwangalla ni kijana mwingine mwenye kuthubutu, lakini
wachambuzi wanasema muda wake kuwa kiongozi wa nchi bado haujafika,
anahitaji kupikwa kwanza. Vivyo hivyo, kwa mbunge Luhaga Mpina ambaye
kiukweli bado hajafahamika miongoni mwa wajumbe wengi ndani ya CCM.
Kundi la mwisho ni la wengineo ambao wana rekodi tofauti, sifa na nafasi tofauti zinazoweza kuwavusha hadi tano bora.
Kundi la wengine
Hapa wapo wanawake, ambao pia wamejipenyeza kwenye makundi mengine
kutokana na sifa tofauti, mawaziri wa zamani na wa sasa, watendaji
waandamizi wa zamani wa Serikali, wabunge na wanachama wa kawaida.
Kundi la mawaziri linaongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ambaye alisifika
alipoongoza Kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond na baadaye
kuteuliwa kuwa waziri.
Pia, yumo Profesa Sospeter Muhongo, ambaye utendaji wake kwenye Wizara
ya Madini umeifanya CCM iutumie kujinadi hasa kutokana na mradi wa umeme
vijijini. Doa kubwa ni katika sakata la escrow ambalo alituhumiwa kwa
kushindwa kulisimamia vizuri na kusababisha Serikali ikose mapato.
“Profesa Muhongo ni ‘potential’, lakini chama kinataka ushindi. Katika
mazingira kama yale ya escrow huwezi ukamweka mbele hata kama hana
matatizo,” alisema mmoja wa makada wa CCM.
Wanawake wanaoingia kwenye kundi la wengineo ni Ritta Ngowi, Dk Mwele Malecela na Monica Mbega.
UTILITY
Kundi la kifo
1. Profesa Mark Mwandosya
2. Stephen Wasira
3. Frederick Sumaye
4. Edward Lowassa
5. Bernard Membe
6. Mizengo Panda
Kundi mbadala
1. Dk Mohamed Gharib Bilal
2. Jaji Augustino Ramadhani
3. Balozi Amina Salum Ali
4. Dk John Magufuli
5. Dk Asha-Rose Migiro
6. Makongoro Nyerere
Kundi la Vijana
1. January Makamba
2. William Ngeleja
3. Dk Mwele Malecela
4. Luhaga Mpina
5. Mwigulu Nchemba
6. Lazaro Nyalandu
7. Dk Hamisi Kigwangalla
Kundi la wengineo
1. Profesa Sospter Muhongo
2. Dk Harrison Mwakyembe
3. Samuel Sitta
4. Dk Titus Kamani
5. Mathias Chikawe
Mwananchi


0 comments :
Post a Comment