UNAMPENDA MTU WA MTU ILI IWEJE?

JUMAMOSI nyingine mpenzi msomaji wa safu hii tunakutana kuweza kujuzana masuala ya mahaba. Hapa tunawekana sawa, wiki iliyopita tulijifunza namna ambavyo tabia inavyoweza kujenga au kubomoa uhusiano.

Nilieleza kwamba, uzuri wa umbo, sura na vitu vingine vinapaswa kuwa chaguo la pili kwa mwanamke au mwanaume. Chaguo la kwanza linapaswa kuwa tabia njema. Ili uweze kudumu na mtu kwenye uhusiano ni vyema mkasomana tabia, ziwe njema na wote mfanane.

Ukimfuata mwanaume au mwanamke kutokana na mvuto wa sura, utakachoambulia ni maumivu. Uhusiano huo utakuwa na kasoro huko mbele na mara nyingi uhusiano wa aina hiyo huwa hauna maisha marefu pale mtakapokutana na changamoto za maisha.


Wiki hii tunakwenda kuangalia mada nyingine iliyopo hapo juu. Kutokana na sababu nyingi tofauti, watu wengi kwa sasa wanajikuta wakiangukia katika penzi la mtu mwenye mpenzi mwingine. Mwanaume anaangukia katika penzi la mwanamke mwenye mchumba au mume wake.

Vivyo hivyo mwanamke anaangukia katika penzi la mwanaume mwenye mchumba au mke wake. Mapenzi kweli ni hisia. Kutokana na mazingira na mtu unayemuona mbele yako, si kitu cha ajabu ukajikuta umependa mtu wa mtu.

Mfano upo katika matembezi. Ukakutana na mtu, mkashirikiana katika jambo fulani ambalo linaweza kuzaa urafiki wa kawaida na baadaye ni rahisi kugeuka kuwa uhusiano wa kimapenzi.

Bahati mbaya wengi sana wamejikuta wakishindwa kujizuia. Wanaanika hisia zao kwa watu pasipo kujali kwamba tayari wana watu wengine. Mtu anatupia ushawishi, anayeshawishiwa naye anakuwa tayari ameshaguswa na vitu fulanifulani kwa mtu huyo, wanajikuta wamechepuka. Wanaendeshwa na hisia.

Kutokana na umri walioishi na mpenzi au mume wake, wanahalalisha uhusiano wao wa wizi kwa kigezo cha kufanya kwa siri. Mhusika anapanga muda maalum wa kuonana na mchepuko wake. Anampa ratiba ya kupiga simu. Kwamba apige simu wakati wa mchana, usiku anakuwa na ‘mzee’. Usaliti unashika kasi.

Ndugu zangu, kuna kitu cha kujifunza hapa. Kwanza kabisa unapaswa kuelewa kushiriki penzi na mtu wa mtu si sahihi. Ukishaona mtu ana mchumba, mke au mumewe ni vyema ukaheshimu penzi lao. Usijifanye mjuaji wakati matokeo ya penzi hilo jipya huwa ni majuto.

Kwa namna yoyote ile, kumpenda mtu wa mtu kwa kisingizio kuwa mtajificha ni mateso. Mbaya zaidi, asipokukubali, utaambulia maumivu. Yawezekana alikuheshimu, akakueleza fika kwamba ana mtu wake lakini wewe bado unamng’ang’ania. Eti umependa, halafu?

Hata ikitokea amekubali kwa kukupa masharti ya kuiba, bado wewe utakuwa mtumwa. Huwezi kuwa na uhuru na huyo mtu wa mtu. Atakupotezea muda. Furaha ya moyo wako itakuwa nusunusu. Utakutana naye kwa wizi, hata huwezi kufurahia mapenzi. Utapoteza muda bure.

Kwa nini usimtafute au kusubiri ambaye atakuwa ni wako peke yako. Kusafiri na mtu ambaye tayari ana mtu ni sawa na kukaa na bomu ambalo linaweza kulipuka muda wowote. Kuna wakati unaweza kujulikana, ukasababisha mtafaruku kwenye uhusiano wa watu. Unaweza hata kupigwa au kudhalilishwa.

Utamu wa mapenzi ni kuwa huru. Ujiachie kwa mwenzako naye afanye hivyo. Azitawale hisia zako na wewe vivyo hivyo. Asiwepo hata mmoja mwenye shaka na mwenzake. Tofauti na hapo penzi litakuwa ni karaha. Unataka kuonana na mpenzi wako unashindwa kwa sababu wakati huo yupo na mtu wake.

Unataka kumpigia simu, umchombeze kwa maneno ya kimahaba, umfariji usiku, akudekee au umdekee, haiwezekani. Mwenzako anakuwa bize na mtu wake wakati huo. Wewe unaambulia maumivu. Unapopoteza muda mwingi katika kuwaza penzi la mchepuko, ni vigumu kufikiria au kupata mtu wako sahihi.

Usikubali. Amua kuishi na mtu ambaye utakuwa na uhuru naye. Utampata kwa wakati. Ukimuhitaji unamuona. Utamuamini naye atakuamini. Hilo ndilo penzi sahihi la wapendanao ambao wanafurahia uhusiano.

Kwa leo ni hayo tu. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri ya kusisimua!
GPL
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment