\Meneja
Mradi Ruvu chini Mhandisi Emmanuel Makasa akiwaonesha waandishi wa
habari sehemu ya bomba la kusafirisha maji kutoka chanzo cha Ruvu chini
kwenda jijini Dar es salaam.
Sehemu
ya bomba la kusafirisha maji kutoka chanzo cha Ruvu chini kwenda jijini
Dar es salaam lilivyozamishwa chini tayari kwa kusafirisha maji ambayo
yatawanufaisha wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kwa matumizi
mbalimbali.
Baadhi ya mitambo ya kusafisha maji ambayo yamesafishwa tayari kwa matumizi ya wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani.
Baadhi ya waandishi wa habari na viongozi kutoka Wizara ya Maji wakiwa eneo la chanzo cha maji cha Ruvu Chini.
Fundi
akiendelea na kazi ya kuunganisha na kuchomelea bomba la maji ambalo
litasafirisha maji kutoka Ruvu Chini kwenda jijini Dar es salaam.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
…………………………………………………………………………………………….
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA)
inaendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu ya maji ili kuwanufaisha
wakazi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kupata maji kwa mahitaji yao
ya kila siku.
Mioundombinu hiyo inayoboreshwa ni pamoja na bomba la Ruvu
Chini lenye urefu wa Jumla ya km 55 ambapo hadi sasa km 52.6
zimekamilika na zimebaki km 2.4 ili kukamilisha mradi huo ambao
utasaidia kusimamia moja ya sentensi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya “Kuwatua akina mama ndoo za
maji kichwani”
Ili kufikia azma hiyo ya kuwapatia maji safi na salama
wakazi wa mikoa hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA,
Romanus Mwang’ingo alisema kuwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini na
ujenzi wa bomba kuu kutoka Ruvu Chini hadi matanki ya Chuo Kikuu cha
Ardhi ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la maji katika jiji la Dar es
salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kabla ya
waandishi hao kwenda kujionea hatua iliyofikiwa, Mwang’ingo alisema kuwa
ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2016 na
kuondoa adha ya maji kwa wananchi na kuwaunganishia wengine ambao
hawakuwa na huduma ya maji.
“Tumelazimika kufikia hatua ya kupanua huduma ya
upatikanaji wa maji katika mikoa ya Dar es salaa na Pwani kutokana na
ongezeko la watu kulingana na sensa ya watu ya mwaka 2012, mkoa wa Dar
es salaam una jumla ya zaidi ya watu milioni 5 ambao watatumia maji
zaidi ya lita milioni 5 kwa siku”,
“Katika upanuzi huo, kumekuwa na changamoto ya makazi ya
watu kuwa ndani ya mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 katika mahakama
mbalimbali katika maeneo hayo ikiwemo mahakama ya ardhi, hadi sasa
DAWASA imeshinda kesi 13 na kupewa haki ya kutumia njia hiyo kukamilisha
upanuzi wa mradi” alisema Mwang’ingo.
Kwa mujibu wa Mwang’ing’o kesi nne bado zipo mahamani na ambazo zimefikia hatua mbalimbali kulingana na taratibu za kimahakama.
Lengo la mradi huu ni kuongeza uzalishaji wa maji kutoka
lita milioni 182 hadi 270 kwa siku. Mradi ambapo awamu itakayofuata ni
lita milioni 360 kwa siku.
Chanzo cha maji cha Ruvu Chini ndiyo chenye kiwango kikubwa
ambacho kina wapatia maji wakazi wa Dar es salaam kwa zaidi ya asilimia
75 ikilinganishwa na asilimia 25 kutoka Ruvu Juu.
Mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini unalenga kuongeza
uzalishaji maji na kuwahudumia wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ)
Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani
Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Dar
es salaam ni Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu, Goba,
Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza,
kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo, Vingunguti, Buguruni,
Kariakoo na Ilala.


0 comments :
Post a Comment