Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es
Salaam Kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2015 ambao
umepanda hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 kwa mwezi
Septemba, 2015.
Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es
Salaam Kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2015 ambao
umepanda hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 kwa mwezi
Septemba, 2015. Kulia kwake ni Mtakwimu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Muhdin
Mtindo. (PICHA NA VERONICA KAZIMOTO)
Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam.
MFUMUKO
wa bei wa Taifa kwa mwezi Oktoba, 2015 umeongezeka hadi kufikia
asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 mwezi Septemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii,Ephraim Kwesigabo amesema kuongezeka
kwa Mfumuko wa Bei kumesababishwa na kupanda kwa bei za bidhaa na
huduma zingine za kijamii ikiwemo chakula na nishati.
“Kupanda
kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2015 kumechangiwa na ongezeko la
bei za vyakula kama vile Mchele ambao umeongezeka bei kwa asilimia 0.8,
unga wa muhogo umeongezeka hadi asilimia 0.7, nyama kwa asilimia 0.8,
samaki kwa asilimia 5.5, ndizi za kupika asilimia 0.7 na choroko kwa
asilimia 0.9”, amesema Kwesigabo.
Bidhaa
zisizokuwa za vyakula kama vile vitambaa kwa ajili ya nguo za kike
zimepanda kwa asilimia 1.6, viatu vya kiume asilimia 1.1, mkaa asilimia
1.4 na gharama za kupata ushauri kwa daktari pia zimepanda hadi kufikia
asilimia 1.4.
Kwa
upande Mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.1
ambao ni ongezeko sawa na mwezi Septemba, 2015. Fahirisi za bei pia
zimeongezeka kutoka 159.04 hadi kufikia 159.17 kwa mwezi Oktoba, 2015.
“Fahirisi
za bei za vyakula vya nyumbani na migahawani iliongezeka kidogo hadi
kufikia asilimia 10.0 kutoka asilimia 9.4 kwa mwezi Septemba, 2015
ambapo bidhaa zisizokuwa za vyakula zimepungua kidogo kutoka asilimia
1.9 hadi asilimia 1.7 kwa mwezi Oktoba, 2015,” amefafanua Kwesigabo.
Kwesigabo
amesema kuwa Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa
mwezi Oktoba, 2015 umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 2.1 kutoka
asilimia 2.2 kwa mwezi Septemba, 2015.
0 comments :
Post a Comment