Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni
Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Freeman Mbowe
amesema kuwa hawatashiriki shughuli ya kuapishwa kwa Dk. John Pombe
Magufuli inayotarajiwa kufanyika Alhamis, Novemba 5, 2015.
Kauli hiyo ya Mwenyekiti Mbowe aliyoitoa leo, imekuja wakati kukiwa bado
kuna sintofahamu kubwa miongoni mwa Watanzania kuhusu mchakato wa
uchaguzi hususan upigaji kura, ukusanyaji na ujumlishaji wa matokeo
ulivyofanyika hasa katika nafasi ya urais.
"Hatutahudhuria shughuli hiyo ya kumwapisha Magufuli. Tumekubaliana wote
kwenye UKAWA, ndani ya CHADEMA, viongozi wetu, wabunge wetu wote
hawatahudhuria uapishwaji wala sherehe.
"Tumetoa wito kwa wananchi wote, Watanzania wote, wapenda mabadiliko na
wapenda haki wote kwa ujumla kutohudhuria shughuli hiyo," amesema
Mwenyekiti Mbowe.
Mwenyekiti Mbowe amesisitiza kuwa UKAWA, wapenda mabadiliko wote na
Watanzania wapenda haki hawakubaliani na wanapinga mchakato wa uchaguzi
hususan matokeo ya urais ambayo, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi aliyosema
ni mbovu, yakishatangazwa hakuna haki ya kuyapinga katika mahakama
yoyote ile.
"Tunataka nchi na dunia nzima ijue wazi kuwa hatukubaliani na mchakato
wa uchaguzi hasa matokeo ya urais ambayo kwa mujibu wa Katiba yetu
mbovu, Mwenyekiti wa Tume akishatangaza hakuna mahali pa kuyapinga."
"Matokeo ya ubunge au udiwani yanaweza kupingwa mahakamani, lakini kwa
matokeo ya urais Katiba yetu mbovu inawafunga mikono na miguu Watanzania
wote ambao wangependa waone haki imetendeka katika nafasi hiyo,"
amesema Mwenyekiti Mbowe.
"Watawala wamechezea haki ya Watanzania kupiga kura. Kura zimehesabiwa
kama karatasi za kawaida tu. Hujuma dhidi ya matokeo ya wagombea wetu
imehujumiwa waziwazi. Safari hii hujuma hazikuwa kificho tena. Kila mtu
amejionea matokeo yaliyokuwa na Jaji Lubuva si yale ambaye yalikuwa
yamebandikwa vituoni. Hayakuwa na uhalisia na matokeo yaliyokusanywa na
mawakala. Uchaguzi umefanywa kama ni jambo lisilokuwa na maana yoyote.
Hiyo ni hatari sana kwa taifa lolote linalotaka kukuza demokrasia kama
mojawapo ya nguzo za maendeleo. Hatuwezi kukubali kufika huko," amesema
Mbowe.
Aidha, Mwenyekiti Mbowe ameongeza kusema kuwa vyama vinavyounda UKAWA
vimeitisha kikao cha Wabunge wateule wote wa vyama hivyo ambao
watakutana Alhamis, saa 4 asubuhi, jijini Dar es Salaam.
Imetolewa leo Jumatano Novemba 3, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
0 comments :
Post a Comment