……………………………………………………………………………………………
Na. Nyakongo Manyama- MAELEZO.
Dar es salaam.
Wito umetolewa kwa wananchi kote
nchini kuyatumia maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani ambayo
huadhimishwa kila ifikapo Desemba 1 ya kila mwaka kupima afya zao ili
kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.
Akizungumza na waandishi wa Habari
leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya
Kudhibiti UKIMWI nchini Tanzania Dkt. Fatma Mrisho amesema Siku ya
Ukimwi Duniani nchini itaadhimishwa kwa kuwahimiza wananchi kujitokeza
kwa wingi kupima afya zao na kupata elimu ya kujikinga na maambukizi
ya ugonjwa huo.
Ameeleza kuwa maadhimisho ya
mwaka huu yataambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo za Utoaji wa
Elimu ya Afya na Upimaji wa hiari wa VVU katika maeneo mbalimbali kote
nchini kupitia vituo vitakavyowekwa, Kufungua kituo cha maarifa cha
udhibiti UKIMWI eneo la Manyoni mkoani Singida ambayo ni njia kuu
kuelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za Jirani za Burundi na Rwanda.
Ameongeza kuwa Tume kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali itaendesha mikutano ya kitaalam kuhusu
UKIMWI, Zoezi la upimaji wa hiari wa VVU kwa wananchi, Kupokea tamko
litakalotolewa na Baraza la Watu wanaoishi na VVU pamoja na Uzinduzi wa
taarifa ya tathmini ya Sheria zinazotumika zinazohitaji kurekebishwa
zinazozuia malengo ya sifuri 3.
Aidha Tume itapokea taarifa ya
hali ya maambukizi ya VVU duniani itakayotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa Ban Ki Moon kuhusu dunia na mapambano dhidi ya VVU.
Dkt. Fatma amefafanua kuwa mgeni
rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pamoja na
mambo mengine atazindua Mfuko wa UKIMWI ambao utakuwa chachu ya
kupunguza maambukizi ya VVU nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
ufuatiliaji na tathmini kuhusu UKIMWI wa TACAIDS Dkt.Jerome Kamwela
amesema kuwa kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kwa mujibu wa takwimu za
mwaka 2011/2012 kimepungua na kufikia asilimia 5.3 huku mikoa ya nyanda
za juu kusini ya Njombe, Iringa na Mbeya ikiongoza kwa kuwa na
maambukizi zaidi na mikoa ya Manyara, Tanga na Lindi ikiwa na
maambukizi ya chini ya asilimia mbili.
Dkt. Kamwela amesema kuwa
maambukizi ya VVU ni mengi hasa kwa kundi la watu wenye umri wa miaka
19-24 huku makundi ya wanaojidunga, wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia
moja, wanawake wanaofanya biashara ya ngono yakiendelea kuwa katika
hatari ya kuathiriwa zaidi na maambukizi ya VVU.


0 comments :
Post a Comment