Askari wa Jeshi la Polisi wa wilaya ya Arusha na
vikosi vingine wakiwa wanamsikiliza Afisa Masoko wa URA SACCOS toka
makao makuu Mkaguzi wa Polisi Shabani Jumbe alipokuwa anatoa elimu hiyo
katika ukumbi wa bwalo la Polisi uliopo jijini hapa. (Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mmoja wa wanachama cha Ura
saccos CPL Ezekiel akiuliza swali lililokuwa linamtatiza kwa muda mferu
ambalo baadae lilijibiwa vizuri na Afisa Masoko huyo toka makao makuu
(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mkuu wa kituo kikuu cha Polisi
Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Thomas Mareko akitoa ufafanuzi
kwa askari waliohudhuria kikao hicho juu ya Ura Saccos kulia kwake ni
Mkaguzi wa Polisi shabani Jumbe ambaye pia ni Afisa Masoko wa chama
hicho. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Baadhi ya askari wakiwa wanajaza fomu za Ura
Saccos kwa ajili ya kujiunga na chama hicho mara baada ya kupata elimu
iliyoeleweka toka kwa Afisa Masoko toka Makao makuu Mkaguzi wa Polisi
Shabani Jumbe. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
………………………………………………………………………………………………………………
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Ikiwa tunauaga mwaka 2015 na
kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 masaa machache yajao baadhi ya askari wa
Jeshi la Polisi Mkoani hapa wanaonekana kufurahia baada ya wengi wao
kupata elimu ya Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo Ura Saccos
iliyokuwa inatolewa na Afisa Masoko na uelimishaji wa Chama hicho toka
Makao Makuu Mkaguzi wa Polisi Shabani Jumbe.
Elimu hiyo iliyotolewa na Afisa
Masoko huyo, iliwafanya askari zaidi ya 100 wabadilishe mawazo ya
kujitoa kwenye Chama hicho na badala yake walichukua fomu za kujiunga na
Chama hicho kwa ambao hawakuwa wanachama na kwa wale ambao walikuwa
wanachama waliamua kuongeza kiwango cha makato kwa asilimia 50 hadi 90
huku wengine wakiendelea kupiga simu kwa msimamizi wa Ura Saccos mkoa wa
Arusha PC Said wakitaka fomu za kujiunga na Chama hicho.
Awali akitoa elimu hiyo katika
wilaya za Arumeru, Monduli, Longido na Arusha mjini, Afisa Masoko huyo
alisema tatizo kubwa lililokuwepo ni ufinyu wa elimu kwa wanachama na
wasio wanachama na kufafanua kwamba wameamua kutoka ofisini na kuwafuata
mikoani kwa lengo la kuwaelimisha ili waone umuhimu wake.
Alisema wanachama wengi
walikuwa hawajui sababu zinazosababisha kupata mikopo midogo ndani ya
Chama hicho kwamba zinatokana na kiasi cha Akiba wanazoweka kwa mwaka
kuwa ni kidogo huku akisema wengi wao wanaweka elfu kumi kwa mwezi.
“Sasa mfano utakuta mwanachama
anaweka Tsh. 10,000/= Kwa mwezi ndani ya mwaka mmoja anajikuta ana Tsh
120,000/= alafu baada ya miaka mitatu anaomba mkopo hivi unafikiri
utapata kiasi gani”? Alihoji Afisa Masoko huyo Shabani Jumbe ambaye pia
ni Mkaguzi wa Polisi.
Alisema Chama hicho kwa sasa
kimeweka utaratibu wa kumwekea Mwanachama 3% kwa kila laki tano ambayo
atakuwa ameweka akiba ndani ya chama hicho ambayo inaitwa riba juu ya
Akiba.
Akitoa ufafanuzi juu ya
utaratibu wa Mwanachama kutoa Akiba yake ndani ya siku 90 na si chini ya
hapo alisema hii inatokana na idadi ya wanachama wanaochukua mikopo
kuwa kubwa lakini pia inatoa fursa ya kukusanya madeni toka kwa
wanachama wengine waliokopa.
“Wanachama wengi wanashindwa
kutofautisha kati ya Akiba na Amana ambapo kwenye Amana mwanachama
anaweza kutoa fedha yake wakati wowote na haina notisi ya siku 90 lakini
kwenye Akiba utaratibu wetu ni siku 90 lakini pia karibu askari 21,000
kwa mwezi wanachangia Tsh 10,000 hali ambayo inakwamisha uwezo wa chama
kukua na kusababisha kushindwa kutoa mikopo mikubwa kwa wanachama”.
Alisema Afisa Masoko huyo.
Alisema mbali na kuweka akiba
kwenye chama hicho lakini pia wanachama wanatakiwa wawe wananunua hisa
zaidi ya zile za msingi ambazo ni 20 lakini tu zisizidi 20% ya hisa zote
za chama hicho ili kuondokana na hali ya uchangiaji tu bali pia wawe
wamiliki wa sehemu ya chama na mwisho wa mwaka kupata gawio.
Alisema uwepo wa Chama hicho
ambacho kwa sasa kina wanachama wanaokadiriwa 34,000 kimesaidia kuweka
usimamizi wa nidhamu ya fedha Kwani ni watu wachache wenye uthubutu wa
kuwa na utamaduni wa kuweka Akiba kila mwezi na kuongeza kwamba mpaka
sasa toka mwaka 2007 kimetoa mikopo kwa wanachama wake kiasi cha Tsh.
82.3 bilioni.
Naye Mkuu wa kituo kikuu cha
Polisi cha Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Thomas Mareko ambaye
kitaaluma ni Mhasibu aliwataka askari kuongeza viwango vya akiba zao
hali ambayo itawasaidia kupata mikopo mikubwa na pia kunufaika na riba
ya aslimia tatu ya kila mwezi kwa watakaoweka kuanzia Tsh. 500,000/=.
Alisema awali askari walikuwa
na wasiwasi juu ya Chama hicho lakini baada ya elimu walielewa hivyo
aliwataka wachangamkie fursa hiyo ya kupata mikopo yenye riba nafuu.
Kwa upande wao baadhi ya askari
waliopata elimu hiyo kutoka wilaya mbalimbali za Mkoa huu walisema
wameweza kubadilishwa mawazo yao ya kutaka kujitoa kwenye chama hicho na
hivyo wameamua kuongeza akiba hali ambayo itasaidia kuinua uchumi wao
siku za usoni.
“Nashukuru sana kwa Inpekta
Shabani Jumbe kutoa elimu hii binafsi nimeifurahia na kuongeza ufahamu
kwa upande wangu hali iliyonipa hamasa ya kuchukua fomu na kuongeza
akiba yangu toka 10% hadi 50% kwa mwezi”. Alisema Asia Matauka ambaye ni
Mkaguzi wa Polisi na kushauri kwamba wajenge matawi katika mikoa yote.
“Baada ya kupata elimu
nimegundua kwamba Chama hiki cha ushirika ni chama muhimu sana kwa
askari na mimi nimeamua kuongeza akiba yangu toka elfu 10 hadi elfu 80
kwa mwezi” .Alisema D/C Anzelim toka wilaya ya longido.
0 comments :
Post a Comment