Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiongea na watumishi wa Tume ya Mipango alipowatembelea kwa kusudi la kuwaaga.
Baadhi ya wafanyakazi wa Tume ya
Mipango wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango
alipowatembelea kwa lengo la kuwaaga.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango akisaini kitabu cha wageni baada ya kufika katika Tume ya
Mipango. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji Bi. Florence Mwanri.
…………………………………………………………………………………………………
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango ameiagiza Tume ya Mipango kufanya utafiti kuhusu mapato ya
Serikali na namna ya kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato.
Amesema Tume ya Mipango kama
chombo cha ushauri kwa Serikali kuhusu mipango na uchumi wa nchi, ni
lazima ifanye utafiti juu ya ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuongeza
vyanzo wa kukusanya mapato ya Serikali ili kuiwezesha Serikali
kuwahudumia wananchi wake.
“Serikali isipokusanya
kodi kwa ufanisi haiwezi kuwahudumia wananchi hivyo, ni lazima kodi
ikusanywe ipasavyo ili kuiwezesha kujiendesha” alisema.
Dkt Mpango aliyasema hayo
alipokutana na wafanyakazi wa Tume ya Mipango kwa lengo la kuwaaga baada
ya kuteuliwa na Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt
John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Waziri wa Fedha amesema mianya
yote ya ukwepaji kodi ni lazima izibwe ili kuiwezesha Serikali kukusanya
mapato ya kutosha suala ambalo litairahisishia utoaji wa huduma za
msingi kwa wananchi.
Amesema Serikali haiwezi kutegemea kila kitu kutoka kwa wafadhili wakati nchi ina rasilimali za kutosha hivyo.
Dkt. Mpango amesema Tume ya
Mipango ni lazima iongoze nchi kuelekea katika uchumi wa viwanda ambavyo
vitafanya pato la taifa kuongezeka na kutoa ajira kwa wananchi.
“Sisi kama wataalamu tunatakiwa
kuiongoza nchi katika kufikia kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka
2025 jambo ambalo linawezekana” alisema.
Waziri pia amesema ni lazima tujenge uchumi imara na madhubuti utakaowezesha kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi.
“Serikali ya Awamu ya Tano
imedhamiria kuboresha ufanisi na utendaji wa Serikali kwa ujumla hivyo
ninyi kama wataalamu mna mchango mkubwa katika kutimiza hilo” alisema.
Tume ya Mipango ni chombo
mahususi cha fikra rejea na ushauri kwa serikali kuhusu sera na mikakati
ya maendeleo, kiuchumi na kijamii ambao unaambatana na ufuatiliaji na
utathmini wa mwenendo wa uchumi nchini.
Aliwataka wafanyakazi wa Tume ya Mipango kufanyakazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa ili kuimarisha utendaji Serikalini.
0 comments :
Post a Comment