HALMASHAURI
ya jiji la Dar es Salaam imeahirisha uchaguzi wa meya wa Jiji uliokuwa
ufanyike leo, mpaka hapo tarehe itakapotangazwa baadaye.
Mkuu
wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano na Umma wa Jiji, Gaston Makwembe
alisema uchaguzi huo uliokuwa ufanyike leo saa nne asubuhi katika ukumbi
wa Mmikutano wa Karimjee, umeahirishwa.
Alisema
tarehe ya uchaguzi huo itapangwa baadaye na taarifa zitatolewa kwa
wananchi kupitia vyombo vya habari bila kueleza sababu ya kuahirishwa
kwa uchaguzi huo.
Uchaguzi
huo unatarajiwa kuwa na mvutano wa aina yake kati ya vyama vinavyounda
na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Diwani
wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita (Chadema) ndiye atapeperusha bendera
ya Ukawa huku mgombea wa nafasi ya Naibu Meya akitarajiwa kutoka CUF.
Chama Cha Mapinduzi (CCM ) wakiwakilishwa na Diwani wa Kinondoni, Yusuph
Omary Yenga.
Inaelezwa
kuwa Ukawa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na
kuwa na idadi kubwa ya madiwani ambapo wanaizidi CCM kwa jumla ya
madiwani 13.
Ikiwa
Ukawa watafanikiwa kutwaa jiji hilo, itakuwa ni mara ya kwanza katika
historia ya Tanzania kwa wapinzani kuliongoza tangu kuasisiwa kwa mfumo
wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Awali,
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alitoa mwito kwa Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusimamia uchaguzi huo
kwa amani na haki ili usifanyike kama wa kumtafuta meya wa Ilala na
Kinondoni uliokuwa na mizengwe mingi.
0 comments :
Post a Comment