Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali haitavumilia usimamizi mbovu wa michezo na usiojali maslahi ya taifa huku akimuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kulifanyia tathmini Baraza la Michezo la Taifa.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge, ambapo amesema endapo waziri huyo atakuta baraza hilo halitimizi wajibu wake, afanye uamuzi wowote kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kulivunja na kuliunda upya.
“Namuagiza waziri alifanyie mapitio Baraza la Michezo la Taifa na kama akiona haliko sawa, anao uwezo wa kulivunja haraka kwa maslahi ya taifa”. amesema Waziri Mkuu
Amesema serikali ya awamu ya tano inatambua umuhimu wa michezo nchini kama sehemu ya kujenga afya na ajira kwa vijana, na ndiyo maana imejitolea kwa kiasi kikubwa katika kuiwezesha timu ya taifa ya vijana ‘Serengeti Boys’ katika michuano ya Afrika kwa vijana nchini Gabon.
Ameliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha linaiendeleza timu hiyo kwa kuwatunza wachezaji na kuongeza mkazo katika uwekezaji kwenye soka la vijana.
Kuhusu michezo mashuleni, Waziri Mkuu amesema serikali imerudisha michezo mashuleni (UMISETA na UMITASHUMTA) huku akiwapongeza wadau wote walioshiriki katika maandalizi na uendeshaji wa michezo ya mwaka huu iliyofanyika Jijini Mwanza.
Katika kuendeleza michezo kuanzia mashuleni, amesema serikali itatenga shule mbili katika kila mkoa ambazo zitakuwa ni kwa ajili ya michezo pekee, pamoja na kuanzisha ufundishaji rasmi wa michezo kama somo katika shule zote za serikali nchini
0 comments :
Post a Comment