Baadhi ya watakwimu ambao ni wanachama wa Chama cha Takwimu Tanzania (TASTA) wakifuatiliakwa umakini hotuba ya mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt.Servacius Likwelile katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Watakwimu Tanzania Bara(TASTA) uliofanyika jana jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC). Mkutano huo ulihudhuriwa na watakwimu zaidi yamia tatu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL GHULA-NBS)
SERIKALI YAHIMIZA MATUMIZI YA TAKWIMU RASMI
NA EMMANUEL Ghula – NBS
SERIKALI imehimiza wadau wa Maendeleo, Taasisi na Mashirika mbalimbali kutumia takwimu rasmi katika kupanga, kutekeleza na kutathimni programu za maendeleo.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Watakwimu Tanzania (TASTA), uliofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile amesema ni vyema wadau wa maendelo, taasisi na mashirika kutumia Takwimu rasmi ili kupata matokeo bora katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Leo mmejumuika hapa pamoja watakwimu kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu kwa lengo la kujadili na kupanga mipango mbalimbali ya chama chenu pamoja na mustakabali wa tasnia ya Takwimu kwa ujumla.
Takwimu rasmi ni macho katika kupanga, kutekeleza na kutathmini miradi ya kimaendeleo. Natoa wito kwa wadau, taasisi na mashirika mbalimbali kutumia Takwimu rasmi zinazotolewa na watakwimu ili kupata matokeo yaliyo bora katika utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo,” alisema Dkt. Likwelile.
Dkt. Likwelile alisema ikiwa upangaji wa mipango ya maendeleo kwa wananchi hautazingatia matumizi ya Takwimu rasmi, kuna athari kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yeyote ile duniani hususani katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs).
Aidha, alisema kuwa ni vyema wananchi na wadau wengine kufuata Sheria ya takwimu Na. 9 ya mwaka 2015 inayoipa mamlaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuanzisha Mfumo wa Takwimu nchini pamoja na kuratibu na kusimamia shughuli zote za ukusanyaji wa takwimu rasmi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa alisema wamekutana kwa lengo la kuboresha na kuimarisha tasnia ya Takwimu na maslahi ya watakwimu.
“Mkutano huu ni wa watakwimu kutoka Tanzania Bara ambapo tupo hapa kwa lengo la kujadiliana ni jinsi gani tunaweza kuwa na umoja madhubuti na wenye nguvu pamoja na kuimarisha tasnia hii ya Takwimu ukizingatia Takwimu ndio msingi wa maendeleo,” alisema Dkt. Chuwa.
Alisema kupitia chama cha watakwimu Tanzania wataweza kuifanya tasnia hii kuwa na nguvu pamoja na kuboresha utendaji kazi wa watakwimu katika maeneo yao mbalimbali walipo ikiwemo katika Halmashauri, Wilaya na Mikoa.
Mkutano Mkuu wa watakwimu Tanzania Bara ulifanyika jana katika ukumbi wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) na kuhudhuriwa na watakwimu zaidi ya mia tatu kutoka mikoa yote ya Tanzania bara.
Mkutano huo umefanyika kwa siku mbili kuanzia Januari 28 hadi 29, 2016.
|
0 comments :
Post a Comment