Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza
na baadhi ya watendaji wa Mgodi wa Makaa ya Mawe ya Ngaka mara baada ya
kuwasili katika mgodi huo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoa wa Ruvuma.
Wengine ni ujumbe aliofuatana nao pamoja na Mbunge wa Mbinga
vijijini, Martin Msuha, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, Kamishna
Msaidizi wa Madini, anayeshughulikia Leseni John Nayopa, Watendaji toka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika
la Maendeleo ya Taifa
(NDC), Ofisi ya Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, baadhi ya Maafisa toka
Wizara ya Nishati na Madini na EWURA.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo, (kulia) akiwasikiliza
wawakilishi wa wananchi wa Kijiji cha Mtundualo, Wilaya ya Mbinga ambao
walimwomba waziri asikilize malalamiko yao ikiwemo kuhusu suala la
fidia kupisha mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka na ombi la kijiji hicho
kupatiwa umeme. Kwa mujibu wa Meneja wa Tanesco Kanda ya Kusini, Joyce
Ngahyoma, amewahakikishia kuwa ifikapo mwezi Aprili mwaka huu kijiji
hicho kitakuwa kimeunganishwa na nishati ya umeme.
Mkuu
wa Wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, akijadiliana jambo na baadhi ya
Watendaji wa Mgodi wa Ngaka kampuni ya TANCOAL, mara baada ya waziri
kukagua shughuli za mgodi huo na kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu
fidia. Waziri Muhongo amezitaka pande mbili kati ya Kampuni, Halmashauri
na wananchi kukutana ili kujadili na kukubaliana kuhusu masuala kadhaa
yakiwemo fidia na uhifadhi wa mazingira.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akimsikiliza
Mwendeshaji Mitambo wa kituo cha kufua umeme cha Tulila kinachomilikiwa
na Shirika la Wabenedictin wa Mtakatifu Agnes Chipole, Sister Maria
Katani (OSB),. Wengine wanaofuatilia nia Meneja wa Tanesco Kanda ya
Kusini, Joyce Ngahyoma na Afisa toka Wizara ya Nishati na Madini,
Christopher Bitesirigwa.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akisalimiana na
Mfadhili wa Kituo cha Kufua umeme kinachomilikiwa na Watawa wa Shirika
la Shirika la Wabenedictin wa Mtakatifu Agnes Chipole, Albert Cock
(kushoto). Kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha kilowati 800 kipo Kata
ya Magarura, wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma. Aidha, sehemu ya umeme
unaozalishwa na kituo hicho unasambazwa Songea, JKT Mlale na Chuo cha
Maendeleo ya Jamii Mlale. Vilevile, Kituo hicho kipo katika hatua za
ujenzi wa kituo kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha megwati 7.5.
Meneja
wa Tanesco Kanda ya Kusini, Joyce Ngahyoma akimweleza jambo Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati alipotembelea kituo
cha mwekezaji binafsi cha Kufua umeme kinachomilikiwa na Familia ya
Andoya, Wilaya ya Mbinga. Mradi huo wa Mbangamao unazalisha megawati
0.2, huku malengo ni kufikia megawati 2. Anayemsikiliza nyuma yake ni
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ruvuma, Patric Lwesya, wengine ni ujumbe
uliofuatana na Waziri.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika picha ya pamoja
na Watawa wa Shirika la Shirika la Wabenedictin wa Mtakatifu Agnes
Chipole, Mfadhili wa Kituo hicho cha kufua umeme Albert Cock, ujumbe
aliofuatana nao wakiwemo Maafisa toka Wizara ya Nishati na Madini,
EWURA, Shirika la Umeme Nchini, Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC),
Uongozi wa Wilaya ya Mbinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini Martin Msuha,
Uongozi wa Kijiji, Wakandarasi wanaojenga kituo cha kuzalisha umeme cha
megawati 7.5, na baadhi ya wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Baadhi
ya Maafisa Kutoka Wizara ya Nishati na Madini (Mbele) na ujumbe
uliofuatana na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
(nyuma) kutembelea kituo cha Kufua umeme cha Tulila kinachomilikiwa na
Watawa wa Shirika la Wabenedictin wa Mtakatifu Agnes
Chipole,wakiangalia maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Bwawa la kufua
umeme. Imeelezwa kuwa, kukamilika kwake kutawezesha uzalishaji wa umeme
wa kiasi cha megawati 7.5.
……………………………………………………………………………………………………………..
Asteria Muhozya na Rhoda James, Mbinga
Serikali imesema itahakikisha inafanya Makaa ya Mawe yanakuwa chanzo kingine kikubwa cha uzalishaji umeme Nchini
Hayo yameelezwa na Waziri wa
Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alipotembelea Mgodi wa Makaa
ya Mawe wa Ngaka unaomilikiwa kwa ubia Kati ya Kampuni ya TANCOAL na
Serikali kupitia shirika la NDC. Mgodi huo upo katika Wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma.
Aidha, ili kufikia lengo hilo
,Prof. Muhongo amesema Serikali itahakikisha inafanya kazi kwa
ushirikiano mkubwa na Mgodi huo ambao Serikali ina umiliki wa hisa ya
asilimia 30 kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) ili kuimarisha
uchumi wa taifa kupitia Makaa ya Mawe.
Ameongeza kuwa, ili kuhakikisha
kwamba Kampuni ya TANCOAL inaendelea kuzalisha makaa na kutumiwa na
viwanda vya ndani, Prof Muhongo amevitaka viwanda vilivyoingia Mkataba
wa mauziano na mgodi huo kuacha kununua Makaa kutoka nje ikiwa makaa ya
Ngaka yanakidhi viwango na ubora unaotakiwa.
“Nimeelezwa Makaa ya Ngaka yana
ubora na kiwango cha hali ya juu na nimeelezwa kwamba kuna baadhi ya
viwanda vimeingia mkataba na Ngaka lakini badala yake wananunua makaa
kutoka nje. Hilo halikubaliki ikiwa makaa ya ndani ya nchi yana ubora
lazima tutumie bidhaa za nyumbani,”amesisitiza Prof. Muhongo.
Kutokana na malalamiko ya Mgodi
kuhusu hali ya Mkataba ya kuuziana makaa kutoafikiana, Waziri Muhongo
ameutaka mgodi huo,NDC,EWURA, Kampuni za Saruji za Dangote, Tanga Cement
na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kukutana Makao Makuu ya Wizara
tarehe 14 Januari,2016, ili kujadili kuhusu suala hilo na pia
kujadiliana juu ya gharama za kuuziana umeme na TANESCO pindi mgodi huo
utakapoanza kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe.
” Umeme wa makaa ya mawe Tanzania
ni lazima. Tutapigana kufa na kupona kuhakikisha tunazalisha umeme kwa
kutumia makaa ya mawe kwa sababu gharama zake zitakuwa nafuu kwa
wananchi na pia umeme huu utachochea ukuaji wa viwanda nchini,”
amesisitiza Prof. Muhongo.
Kadhalika Prof. Muhongo amerejea
kauli yake ya kuwataka wazalishaji umeme hususan wa makaa ya mawe na
vyanzo vingine kuhakikisha wanaiuzia TANESCO umeme wa bei ya chini na
kuongeza “mauziano ya umeme wa makaa ya mawe lazima yafuate viwango vya
kimataifa. Lazima yawe ya gharama nafuu.”
Katika hatua nyingine, Prof.
Muhongo amewataka EWURA kubadilika na kushiriki katika hatua za mwanzo
za majadiliano ya gharama za kuuziana umeme katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali badala ya kusubiri kushiriki katika hatua za mwisho na
kulieleza jambo hilo kuwa ushiriki wao katika hatua za awali unawezesha
majadiliano na makubaliano kufanyika kwa haraka.
Aidha, Prof. Muhongo amechukua
fursa hiyo kuzitaka Mamlaka chini ya wizara kuzingatia suala la usawa na
namna Serikali inavyonufaika na makubaliano ya utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya kitaifa kwa kuzingatia kuwa rasilimali ni za nchi , hivyo
taifa linapaswa kunufaika na uwekezaji husika.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Masoko wa
mgodi wa Ngaka, Christopher Temba, mgodi huo unazalisha tani za makaa ya
mawe Laki Tano kwa mwaka lakini lengo ni kufikia tani milioni moja.
Tayari makaa hayo yanasafirishwa
katika nchi za Kenya, Zambia, Malawi na vilevile katika viwanda kadhaa
hapa nchini vikiwemo vya Saruji Tanga Mohamed Enterprises na viwanda
vingine
0 comments :
Post a Comment