Nkupamah media:
Siku chache baada ya kutokea tukio la majangili katika pori la akiba Maswa wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, kuitungua ndege (helikopta) iliyokuwa doria na kuaawa kwa rubani wake Rodgers Gower (37), watu 9 wamekamatwa kuhusika na tukio hilo.
Katika watuhumiwa hao mmoja niMhifadhi wa hifadhi ya taifa ya Ngorongoro kitengo cha Interejensia, ambaye alitajwa kuwa mhusika Mkuu wa kufanikisha tukio hilo sambamba na kukamatwa mganga wa jadi.
Akitoa taarifa mbele za waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa polisi Mkoani Simiyu Lazaro Mambosasa alisema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na jeshi hilo kufanya kazu usiku na mchana kwa kushirikiana na wananchi, pamoja na uongozi wa TANAPA.
Kamanda Mambosasa alisema watuhumiwa wote walikamatwa na kukiri kuhusika na tukio hilo, huku akieleza kuwa msako mkubwa uliofanywa na jeshi hilo mara baada ya tukio kutokea chini ya Mkuu wa upelelezi Mkoa Jonathan Shana.
Alisema katika msako huo baadhi ya watuhumiwa walibainika kuwa kiungo kikubwa kufanikisha tukio hilo kwa kutoa mbinu za uharifu, huku wakijihusisha na matukio ya ujangili kwa muda mrefu.
Aliongeza kuwa baadhi yao walibainika kuwa waganga wa jadi, ambapo walikuwa wakitoa dawa kwa majangili za kuosha silaha, ikiwa ni pamoja na kuosha na kusafisha miili yao ili wasiweze kukamatwa.
Mambosasa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shija Mjika (38), Njile Gonga (28) Mhazabe, Masasi Mandago (48) pamoja na Dotto Pangali (41) , ambao ndio walihusika kutungua helkopta hiyo.
Wengine ni Iddi Mashaka (49) ambaye Kamanda Mambosasa alimtaja kuwaMhifadhi wa hifadhi ya taifa ya Ngorongoro Kitengo cha Intelijensia na ndiye alikuwa kiungo Mkuu wa tukio hilo.
Aliwataja wengine kuwa ni Mapolu Njige (50) ambaye ni mganga wa jadi aiyekuwa anatumika kutoa dawa za kutokamatwa kwa majangili hao, Mwigulu Kanga (40) , Dotto Huya (45) , Pamoja na Mange Balumu.
Aidha Mambosasa alisema kuwa Mtuhumiwa Dotto Pangali alikamatiwa katika wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga mnamo tarehe 7/02/216 na kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake ambapo alikutwa na bunduki aina ya Riffle yenye namba .7209460 CAR Na.63229.
Mkuu huyo wa polisi alisema Mtuhumiwa huyo alikiri bunduki hiyo kutumika katika tukio la kuuawa kwa rubani huyo, ambapo ilibainika kuwa bunduki hiyo inamilikiwa na Mange Magima ambaye pia amekamatwa.
Alisema msako uliendelea nyumbani kwa Pangali na kufanikiwa kukamatwa kwa bunduki nyingine aina ya Riffle Na3478 CAR 458 ikiwa na risasi 6 ambayo ilibainika kumilikiwa na Nghomango Jilala ambaye mpaka sasa hajakamatwa.
Alieleza kuwa jeshi hilo liliendelea kupata taarifa ambapo mnamo tarehe 29/01/2016 walikamatwa Shija Mjika, Njile Gonga, pamoja na Masasi Mandago wakiwa na meno ya tembo 2 yakiwa na uzito wa Kilo 31 yakiwa yamefichwa chini ya daraja katika kijiji cha Itaba.
Aidha Mambosasa alieleza kuwa baada ya kukamatwa kwa wahusika wote ilibainika kuwa bunduki zilizotumika katika tukio hilo zinamilikiwa kihalali na watu ambao waliomba kuzimiliki kwa ajili kujilinda.
“Mbali na tukio hilo bunduki nyingi wamiliki wake wanawaazimisha majangili kwa ajili ya kutumika kwa uhalifu pamoja na kuua wanyama ndani ya hifadhi…lakini na hao wamiliki wanalipwa pesa baada ya uhalifu kufanyika” ,alisema.
Alisema baada ya kubaini hilo kulifanyika msako mwingine kwa wanaomiliki silaha, ambapo alisema asilimia kubwa wanaishi karibu na hifadhi, na jumla ya bunduki 27 zimekamatwa na mara baada ya uchunguzi wamiliki watarudishiwa.
“Tunajiandaa kupeleka zuio la silaha mahakamani ili kubaini kama wana sifa za umiliki…lakini mbali na hilo sasa kutaanzishwa oparesheni kwa watu wote wanaomiliki silaha hasa maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuwanyanganya”, alisema.
Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa upelelezi juu ya tukio hilo umekamilika na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani leo Jumanne ili kujibu tuhuma zinazowakabili, ambapo alioomba mahakama kuharakisha hukumu kwa vile uchunguzi umekamilika.
Kwa upande wake Mhifadhi mkuu wa Serengeti William Mwakilema amelipongeza jeshi la polisi ambapo amesema tukio hilo lilipotokea liliwasikitisha sana kwani hasara ilipatikana kutokana na kutunguliwa kwa helkopta.
Mnamo tarehe 29/01/2016 saa 11:30 jioni katika eneo la Gululu lililopo ndani ya hifadhi ya Maswa kata ya Mwangudo wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, majangili waliipiga risasi ndege (helkopta) 88HFCG iliyokuwa doria na kusababisha kifo cha rubani wake Rodgers Gower (37) raia wa uingereza huku Mwenzake Nicholas Beste (43) raia wa Afrika Kusini akinususrika kifo.
0 comments :
Post a Comment