Mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete Asema CCM Ilisikitishwa Sana na Uamuzi wa ZEC Kufuta Uchaguzi Zanzibar

Nkupamah media:

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza rasmi kuachia kiti hicho kabla ya mwezi Februari mwakani, huku akisema CCM imesikitishwa na uamuzi wa ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar.

Dkt Kikwete ambaye pia ni Rais wa awamu ya nne wa serikali ya Jamhuri ya Tanzania, ametoa tamko hilo leo katika sherehe za miaka 39 ya chama hicho zilizofanyika katika uwanja wa Namfua mjini Singida, ambapo yeye ndiye aliyekuwa mgeni Rasmi.

Katika hotuba yake, Dkt Kikwete amewaeleza wana CCM waliofurika kiwanjani hapo kuwa hizo ndizo zitakuwa sherehe zake za mwisho kwake kuhudhuria huku akiwa mwenyekiti, kwa kuwa katika sherehe zijazo mwenyekiti wa chama hicho atakuwa ni Rais John Magufuli.

"Hii ni mara yangu ya mwisho kuhudhuria sherehe hizi kama mwenyekiti wenu, Katika sherehe za mwakani, mwenyekiti wenu atakuwa ni Rais John Magufuli"

Chama hicho kinataraji kufanya maadhimisho yake ya miaka 40 ya kuzaliwa kwake mwezi Februari mwaka 2017 mwaka ambao pia ni wa uchaguzi mkuu wa chama hicho kwa mujibu wa katiba yao.

Kuhusu Uchaguzi mkuu wa Zanzibar, Kikwete amesema wao kama CCM hawakupenda uchaguzi huo urudiwe kwa kuwa walikuwa wana uhakika wa ushindi, na tayari walikuwa wanajiandaa kusherehekea ushindi mnono, lakini wanalazimika kukubaliana na maamuzi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwa hawana namna nyingine.

“Tulikuwa tumejiandaa kushangilia, lakini Tume wakasema kuwa uchaguzi unafutwa kwa kuwa kulikuwa na dosari kubwa, tukasikitika sana lakini kwa kuwa tume wameamua, tukashauriana na wenzetu wa Zanzibar, tukaona ni bora kukubali kurudia uchaguzi huo, lakini hatukupenda”

Amewataka wana CCM wote visiwani Zanzibar kujiandaa na uchaguzi siku ya Machi 20, mwaka huu na kwamba wahakikishe wanatunza shahada zao kwa ajili ya kuchagua wagombea wa CCM.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio ya chama hicho katika kuwaletea watanzania maendeleo ambapo amesema katika miaka yake 39, chama hicho kimefanikisha mengi ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.

Pia amezungumzia mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo licha ya kukiri kuwa chama hicho kilikuwa kwenye wakati mgumu, amesema bado kiko imara, na kitaendelea kuwa imara.

Amesema licha ya baadhi ya watu kukitabiria kifo chama hicho, watanzania bado wameendelea kukiamini na kukipa ushindi wa kishindo huku akitolea mfano ushindi ambao chama hicho kimeupata katika ngazi ya urais, udiwani, na ubunge mwaka 2015.

“Katika ubunge sisi tumepata asilimia 73 ya viti vyote vya ubunge wa majimbo, na hata katika udiwani tumeshinda asilimia zaidi ya 73 katika kata zote, nashangaa kuna watu wanadai kwamba eti CCM haipendwi, yaani hata hesabu zinawashinda..” Amesema Kikwete.

Akizungumzia utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano, Dkt Kikwete amempongeza Rais Magufuli kwa kufanya yale aliyotumwa katika Ilani ya CCM na kuahidi kumpa ushirikiano ili ayafanikishe yote yaliyomo katika ilani hiyo.

Amewakosoa watu wanaodai kuwa Magufuli hatekelezi Ilani ya CCM bali ya vyama vingine na kusisitiza kuwa kila jambo linalofanywa na serikali hiyo limo ndano ya ilani ya CCM.

Kikwete ametolea mfano suala la kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kushughulikia rushwa na wahujumu uchumi na kusema kuwa suala hilo limo ndani ya ilani ya CCM, na wala sio jambo la kuzuka.

Amesema wanaodai Magufuli anatekeleza sera zao wameishiwa na hawana la kuzungumza tena.

"Watani zetu wanasema anatekeleza mambo yao, wamekosa ya kusema wanasubiri akija bungeni watoke, watu wazima hovyooo"

Pia amewataka wanachama wa CCM kuchagua viongozi bora na watakaoweza kukijenga upya chama hicho katika uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika mwakani , huku akiwataka wajiandae kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi ujao, tumemaliza wa mwaka 2015 tuanze kujiandaa na uchaguzi wa 2020
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment