Nkupamah media:
Huku kukiwa na taarifa kuwa wasaliti wa CCM wanaotarajiwa kutimuliwa
wengi ni watu maarufu hasa viongozi wa ngazi za mkoa, tayari viongozi 21
wa Manyara, wameshatumbuliwa majipu bila ganzi.
Jumla ya
viongozi 21, watatu wakiwa ni wa CCM Wilaya ya Babati Mjini mkoani
Manyara na wengine 18 wa ngazi ya kata, wameshaadhibiwa na Mwenyekiti wa
CCM, Jakaya Kikwete alichokiita kutumbua majipu bila aibu.
Inadaiwa kuwa viongozi hao walikuwa wanamshabikia aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Imedaiwa ushabiki ulisababisha CCM ipoteze jimbo na kata tano kati ya nane za Babati Mjini.
Katibu
wa CCM mkoani Manyara, Ndeng’aso Ndekubali aliwataja waliofukuzwa
uanachama kuwa ni wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa, Cosmas Masauda,
Zulekha Mohamed na mjumbe wa mkoa, Felix Kivuyo.
“Hawa wamefutwa
uanachama baada ya kudaiwa kukisaliti chama kwa kuwapigia kampeni
wagombea wa vyama vya upinzani na kuwaombea kura kwenye Uchaguzi Mkuu,”
alidai Ndekubali.
Februari 24, mwaka huu, Kikwete alipokuwa
akizindua nyumba ya chama hicho Kibaha mkoani Pwani, alisema mwanachama
yeyote aliyekihujumu chama chao kwenye uchaguzi wa mwaka jana,
atatumbuliwa jipu bila aibu.
Kikwete alikaririwa akisema tayari
CCM ina majina ya wasaliti wote na mchakato wa kuwaadhibu unaendelea
kuanzia ngazi ya matawi, kata, wilaya mkoa na Taifa. Alisema viongozi
hao wamekiuka ibara ya 93, kifungu cha 14 ya Katiba ya CCM.
“Halmashauri
Kuu ya CCM mkoa, imewavua nyadhifa viongozi 18 wa ngazi za kata
wilayani Babati Mjini kwa kukiuka maadili, kushiriki ubadhirifu wa fedha
na kukosa uaminifu,” alisema Ndekubali.
Alisema viongozi 18 wa
ngazi ya kata ambao walivuliwa nyadhifa zao na kubaki kuwa wanachama wa
kawaida, ni makatibu wa kata tisa, wenyeviti wa kata nane na katibu
mwenezi mmoja wa kata, wote wa Wilaya ya Babati Mjini.
0 comments :
Post a Comment