Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka
wafanyakazi wa wizara yake kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kutumia sekta ya miundombinu kukuza
uchumi wa nchi na kufungua fursa za kiuchumi.
Akizungumza
katika kikao kazi kilichohusisha Sekta za Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Mbarawa amesema kila mtu afanye kazi kwa umoja, uwazi
na uadilifu ili kufikia lengo la kuanzishwa kwa wizara hiyo na
kujihakikishia nafasi ya kuendelea kuwa mtumishi wa umma.
“Huu
sio wakati wa kufanya kazi kwa mazoea, dunia imebadilika tutumie
teknolojia ya habari na mawasiliano kufanya kazi kwa muda mfupi na kwa
tija”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na
wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusu mikakati
ya uendeshaji wa Wizara hiyo inayojenga Miundombinu ya kisasa ili
kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Amesema
kila mfanyakazi atapewa malengo na atapimwa kulingana na malengo
aliyopewa ili kuona kama utumishi wake unakidhi mahitaji ya Serikali
kuwahudumia watanzania inayojiandaa kuwa nchi ya kipato cha kati.
“Kazi
yetu ni moja tu kuwajengea miundombinu ya kisasa itakayowezesha
Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”, amesisitiza Prof.
Mbarawa.
Prof.
Mbarawa amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi kukutana mara kwa mara
kujadiliana masuala muhimu ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kazi
zinazowakabili.
Katibu
Mkuu (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga akifafanua jambo kuhusu
mikakati ya Ujenzi wa Barabara, Nyumba za Serikali na Huduma za Ufundi
na Umeme katika kikao kazi cha Watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano.
Amesema Wizara hiyo ina andaa mtandao wa video (Video Conference Facility)
utakaotumika kuwaunganisha watumishi wa wizara hiyo nchini kote
kujadili na kuyapatia ufumbuzi masuala mbalimbali ya ujenzi wa
miundombinu hapa nchini.
Aidha
Prof. Mbarawa amewataka Makatibu Wakuu wa wizara hiyo Eng. Joseph
Nyamhanga (sekta ya ujenzi), Eng. Dkt. Leonard Chamuriho (sekta ya
uchukuzi) na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Maria Sasabo (sekta ya mawasiliano),
kuimarisha ushirikiano baina ya watumishi wa sekta hizo ili kuiwezesha
wizara kufanya kazi kama timu moja.
Katibu
Mkuu (Sekta ya Uchukuzi), Eng. Dkt. Leonard Chamuriho akifafanua jambo
katika kikao kazi cha Watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani amewataka wafanyakazi kuwa na maono katika majukumu yao na
kujitathimini kila wakati ili kubaini mafanikio na changamoto na
kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inaundwa na sekta tatu na inasimamia
taasisi 29 zenye muelekeo wa ujenzi na usimamizi wa miundombinu na
inatarajiwa kuiandaa Tanzania kuwa na miundombinu ya kisasa
itakayowezesha kuhimili changamoto za kuwa nchi ya kipato cha kati
ifikapo 2025.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Naibu
Katibu Mkuu (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo akifafanua jambo
katika kikao kazi cha Watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
Watumishi
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakifuatilia kwa makini
hotuba ya Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
wakati wa Kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame akiwa na baadhi ya
Mbarawa na wafanyakazi wa Wizara hiyo mara baada ya kikao kazi jijini
Dar es Salaam.


0 comments :
Post a Comment