AFISA MIFUGO wa kata ya Kakunyu, wilayani Misenyi mkoani Kagera, Bw.Eric Kagoro amenusurika kutumbuliwa jipu kwenye mkutano wa hadhara kuhusiana na sakata la kuruhusu ng’ombe 291 waje kulishwa kwenye ranchi ya mifugo ya Misenyi.
Tukio
hilo limetokea leo mchana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akizungumza na mamia ya wananchi waishio jirani na
ranchi hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye makao makuu ya
ranchi hiyo.
Waziri
Mkuu alimuibua Bw. Kagoro katikati ya mkutano kwa kumtaja jina na
tuhuma zinazomhusu kuhusu mifugo iliyokamatwa. “Afisa Mifugo wa kata
yupo hapa?." Aliuliza Waziri Mkuu. "Wewe ndiyo Eric?” Alipojibu ndiyo
akaulizwa tena:”Nimekujuaje?”
“Nimeambiwa wale ng’ombe waliokamatwa ni wa rafiki yako na wewe ndiye ulitoa kibali
waje kulishwa kwenye ranchi hii. Siyo kazi yako kuruhusu mifugo ya nje
ije kulishwa hapa kwenye ranchi. Kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote
kuingiza mifugo kwenye ranchi ili ipate malisho “
“Leo
Nimekusamehe .Kazi yako ni kuhakikisha mifugo ya kwenye kata hii iko
salama. Kazi yako ni kuwasaidia wafugaji wa kata hii wafuge vizuri na
uhakikishe mifugo yao inakuwa na tija.” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Kwa
upande mwingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa watendaji wa
kata na vijiji kutotumia nafasi zao kuleta migogoro baina ya watu wa nje
na wananchi wanaowaongoza. “Mwenyekiti wa kijiji huna ruhusa ya kugawa kitalu cha ranchi au kuruhusu mtu yeyote akalime ndani ya ranchi”, alisema.
Aliwataka
pia maafisa uhamiaji wawe makini na vyeti vya kuandikisha uraia
wanavyovitoa kwa wananchi wanaoishi mipakani kwani imekuwa ni mianya ya
kuleta migogoro ya ardhi. “Watu wa uhamiaji kuweni makini na CN mnazotoa (CN=Certificate of Naturalisation). Wote wanaoomba CN wanataka blocks tu”
Alitoa agizo kuwa watafutwe watu wote walioingia nchini kwa mgongo wa CN, wakamatwe na kurejeshwa makwao. “Kuna watu wamekuja hapa nchini wakaomba CN lakini wakikaa wanaleta wenzao waje kununua ardhi kwa kutumia mgongo wa CN zao.”
0 comments :
Post a Comment