Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa tareh 25 Oktoba 2015, usalama wa raia wa Zanzibar na mali zao umekuwa katika hali tete.
Hali
hii inatokana na kushuhudiwa kushamiri kwa matukio ya kuogopesha
wananchi na kufurutu ada ukiukwaji wa HAKI ZA BINAADAMU miongoni mwa
wananchi kunakofanywa na vyombo vilivyopewa dhamana ya kuhakikisha
ulinzi na usalama wa nchi yetu raia wake na mali zao.
Katika
siku za hivi kadribuni, hususan baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar (ZEC), Jecha Sali Jecha, kutangaza kinyume na katiba ya
nchi, kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba 2015 na matokeo yake, Zanzibar
imeshuhudia uingizwaji na uingiaji mkubwa wa askari, vifaa na zana nzito
za kivita katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Sambamba
na hayo kumekuwepo kwa askari wengi wa JWTZ wanaorandaranda mitaani
wakiwa na silaha nzito za kivita na operasheni isiyo rasmi ya kuwakamata
na kuwabambikizia kesi wananchi wasio na hatia na hatimaye kuwaweka
katika vituo mbali mbali vya polisi na kuwanyima dhamana hata kwa makosa
ambayo kisheria yanapaswa kudhaminiwa.
Katika
mwezi wa February 2016 huko kengeja wafuasi wa CUF walikamatwa na
polisi na kuwekwa ndani kwa tuhuma ya kuchoma tawi la CCM la eneo hilo.
Polisi walichukuwa hatua hiyo mara tu tukio hilo liliporipotiwa kwao.
Aidha katika mwezi huu wa Machi baadhi ya matawi ya CUF na Baraza za CUF
zilichomwa moto na kuteketea tikitiki.
Taarifa
ya uhalifu huu zlipripotiwa katika vituo vya polisi na RB kuandikwa,
hata hivyo hadi hii leo hakuna yoyote aliyekamatwa kwa tuhuma ya uhalifu
huo. Matukio ya uchomwaji moto na uharibifu wa mali za CUF umetokea
mahala mwingi Unguja na Pemba kama vile Kisauni ambapo ofisi mpya ya CUF
jimbo la Dimani zilizogharimu zaidi ya sh 90m zilichomwa moto tarehe
24/03/2015 na kuteketea. Kwa makusudi kabisa, hata baada ya polisi
kupata taarifa hiyo na kulikagua eneo husika hakuna yeyote aliyetuhumiwa
na kukamatwa.
Mtakumbuka
kwamba tabia hii ya wananchi ambao kwa asilimia kubwa huwa ni CCM au
vyombo vya serikali vilikuwa vikihujumu kwa makusudi mali ya CUF na hata
mali ya serikali kama vile shule, zahanati, visima vya maji nk. Tukio
la Shengajuu la 1996 ambapo watu waliofanya tukio la kcuhoma moto shule,
kutia kinyesi visima walikamatwa wakiwa na petrol, bunduki, mapanga,
madoo ya kinyesi vyote vikiwa usoni ya gari la idara ya usalama wa Taifa
lenye namba za usajili ZNZ 1296).
Baada
ya tukio hilo la kufedhehesha serikali na mapambamo yaliyofuata baina
ya wafuasi wa CUF na wahalifu (usalama wa Taifa), serikali iliwaadhibu
kwa kuwapiga, kuwaibia mali zao, kuwafanyia vitendo vya kinyama na
kuwaweka ndani kwa zaidi ya miezi 9 wananchi wasio na hatia. Hivyo haya
yanayoendelea hivi sasa huko Pemba si mambo mageni hasa katika kipindi
hiki ambapo SMZ imechukia sana kwanini CUF wamegomea kushiriki uchaguzi
batili wa madrudio wa 20/03/2016.
Sisi
CUF tunaamini pasipo na shaka yeyote kwamba matukio ya kuchomwa moto
kwa masikani na matawi ya CCM huko Pemba ama baadhi ya nyumba za watu
binafsi na mali za serikali ni mwendelezo tu wa siasa chafu za chuki
zinazoendelezwa na serikali dhidi ya wananchi wasio na hatia. CUF
imesikitishwa sana na vitendo hivi vya kihuni na visivyoonyesha siasa za
kistaarabu na inalaani vikali na kwa nguvu zote uhalifu huu ambao
unarejesha nyuma ‘spirit’ ya kushindana bila kupigana.
Kwa
upande mwengine, CUF imepokea taarifa kwamba zaidi ya wananchi 30 wengi
wakiwa wafuasi, viongozi na wanachama wa CUF wamekamatwa na polisi na
wameshikiliwa katika vituo mbali mbali vya polisi huko pemba. Utendaji
huu wa Jeshi la polisi umeipelekea Zanzibar kugawika vipande vipande na
kuwa chanzo cha siasa za chuki, uhasama na kusababisha nchi yetu
kushindwa kutekeleza shughuli zake za kimaendeleo.
Kwa
mfano amri ya Mkuu wa Mkoa kaskazini Pemba kupiga marufuku watu
wasitembee baada ya saa mbili za usiku na kwamba atakayevunja amri hiyo
atakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la uzembe na uzururaji ni hatua
nyengine ya SMZ ya kuwahalalilisha na kuwaweka wananchi wa mkoa wa
Kaskazini Pemba katika hali ngumu ya maisha. Amri hii inazuwia hata sala
za Isha na Alfajiri jambo ambalo waumini wa Kiislamu hawatakubaliana
nalo.
CUF
inamtaka Mkuu wa Mkoa uliotajwa hapo juu awache ukereketwa na aendeshe
mkoa kwa hekima, busara, na weledi. Kuongoza watu kwa amri za kidikteta
kumepitwa na wakati. Asome alama za nyakati, aache kutoa amri
zinazopingana na hata haki za binaadamu.
Chama
Cha Wananchi CUF kinaamini kuwa kutokea kwa matukio haya ni mwendelezo
wa njama za CCM zinazoratibiwa na kutekelezwa kimkakati kwa malengo
mahususi ya kuamsha hamasa na kupandisha joto la jazba miongoni mwa
wananchi ili kuhalalisha mpango maalum na kutoa fursa kwa vyombo vya
ulinzi na usalama kutumika kutisha, kukamata, kupiga na kufungulia
mashtaka wananchi wasio na hatia.
Kutokana
na unyeti wake matukio ya uvunjifu wa amani na hatua za ukiukwaji wa
HAKI ZA BINAADAMU, hayapaswi kupuuzwa kwani yanaweza kupelekea
kufanikiwa kwa dhamira mbaya waliyonayo baadhi ya watu katika nchi yetu
wasioitakia mema Zanzibar na kwa hivyo kuathiri umoja wa kimataifa
uliopo uliopatikana kwa gharama kubwa ya jasho la viongozi wazalendo,
Mheshimiwa Rais mstaafu wa Zanzibar Dr. Amani Karume na Katibu Mkuu wa
CUF Maalim Seif Sharif Hamad na uhai wa wananchi wanyonge. Kwa hivyo
sisi katika CUF:
•
Tunavinasihi vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi yetu kukataa katakata
kuingia katika mtego wa mipango miovu ya wanasiasa waliofilisika wenye
lengo la kuleta taharuki miongoni mwa wananchi na kuamsha hamasa na
kupandisha jazba na ghamidha zitakazopelekea kuchafuka kwa hali ya amani
ya nchi yetu. CUF inatoa wito kwa kwa vyombo vyote vya Ulinzi na
Usalama hapa nchini kusimamia amani na utulivu pasi na kuegemea upande
wowote wa kisiasa.
Ni
muhimu vyombo hivyo vikajipambanua na kujijengea heshima na kulinda
imani ya wananchi waliyonayo kwao. Kinyume na haya, vyombo vyetu vya
ulinzi na usalama hasa jeshi la polisi na jeshi la wananchi wa Tanzania
JWTZ, ambalo katika siku za hivi karibuni limeonekana kutumika vibaya,
kufahamu kuwa mustakbali wa utu wa raia, mali zao na amani ya nchi yetu
imo mikononi mwao na watakuwa wa mwanzo kuwajibika endapo jahazi la
amani yetu litakwenda mrama.
•
Tunaziomba Taasisi za kiraia za ndani kuacha woga na badala yake kupaza
sauti zao masikioni mwa viongozi madhalimu kukemea unyanyasaji na
ukandamizaji wa haki za binadamu. Aidha, CUF inaziomba jumuiya za
kimataifa kuendelea kuitazama Zanzibar kwa umakini wa hali ya juu
kufuatilia mwenendo na matukio na kuweka kumbukumbu kwa hatua za baadae
kwa kila anaeonekana kushtadi kuonea wananchi wanyonge kutokana na
nafasi yake katika utumishi wa umma.
•
Tunatoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa,
John Magufuli, kuchukua dhamana ya uongozi kukataa kuhadaiwa na
wasaidizi wake na kukomesha matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi na
usalama vilivyo chini ya amri yake na kudhibiti uhuni wa kisiasa wa
baadhi ya watendaji wa vikosi vya Idara Maalum ya Zanzibar kama Amiri
Jeshi Mkuu wa Tanzania. Kwa la zanzibar, Rais Magufuli hana pa kupenyea
na kwamba atawajibika kutokana na mfumo wa Katiba, sheria na utaratibu
wa kuongoza nchi tuliojiwekea.
•
Tunatambua usumbufu, idhilali na mateso makubwa yanayowapata wananchi
wa visiwa vyote vya zanzibar kufuatla maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba
2015 ya kuikataa CCM na kuamua kufanya mabadiliko katika uongfozi wa
nchi. CUF inawaomba wananchi wote kuendelea na kujipamba na mavazi ya
subira na kuamini kuwa hizi ni hatua za mwisho za CCM kuelekea kufutika
katika nyoyo za wazanzibari na kwamba wananchi wote wausiane katika
kuvumilia na kukataa kuchokozeka kwa lengo la kutunza amani ya nchi yetu
na kufikia malengo yetu ya muda mrefu ya kukamata hatamu za dola ya
zanzibar bila kuathiri wanachi wetu.
•
CUF inawahakikishia wananchi wote kuwa haitarudi nyuma katika mapambano
ya kudai haki ya wananchi na kwamba maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba
2015 yatazingatiwa, kuheshimiwa na hatimaye haki kutamalaki katika
visiwa vya zanzibar. Ni wajibu kwa wazanzibari wote kutambua kuwa giza
nene hufuatiwa na miale ya nuru inayotoa faraja kwa kila mwanandamu.
……………………………….
HAMAD MASOUD HAMAD
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA
MAWASILIANO KWA UMMA
0 comments :
Post a Comment