Nkupamah media:
Waogeleaji wa klabu ya Dar Swim wakipasha viungo moto kabla ya kuingia mashindanoni
Waogeleaji wakipasha viungo kwa staili ya backstroke
Waogeleaji wakipasha jinsi ya kupiga mbizi au ku-dive
………………………………………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu
Klabu maarufu ya kuogelea jijini,
Dar Swim Club imewapongeza waogeleaji wake kwa kufanya vyema katika
mashindano ya taifa ya kuogelea yaliyomalizika hivi karibuni katika
bwawa la Hopac.
Akizungumza jijini jana, Katibu
Mkuu wa klabu hiyo, Inviolata Itatiro alisema kuwa waogeaji wake
wameweza kuboresha muda wa kuogelea na kuiwezesha klabu hiyo kutwaa
nafasi ya kwanza kwa upande wa wanawake kwa kukusanya jumla ya pointi
1,964.50.
Inviolata alisema kuwa kwa upande
wa wanaume, walikusanya jumla ya pointi 1,086.50 na kushika nafasi ya
pili. Alisema kuwa wamefarijika na matokeo hayo kutokana na wao
kuwakilishwa na waogeleaji chipukizi katika mashindano hayo.
“Hii ni faraja kwetu, tumeweka
mikakati ya kukuza mchezo wa kuogelea kwa miaka 10, tunawaogeaji wadogo
sana lakini wana vipaji vya hali ya juu, lakini kutokana na mfunzo
mazuri ya makocha wetu, wameweza kuwashinda waogeleaji wenye umri
mkubwa, kwa kweli wanastahili pongezi,”
“Wakati tunaanza, hatukutegemea
kufikia hatua hii, tuliweza kutwaa medali 94 katika mashindano ya
kuogelea ya Taliss na kushika nafasi ya kwanza na kuwa klabu bora, natoa
wito kwa wazazi ambao wanataka watoto wao kujua kuogelea na kushindana
katika mashindano ya ndani na kimataifa, kujiunga na klabu yetu,”
alisema Inviolata.
Alisema kuwa mafanikio ya klabu
yao yametokana na ushirikiano wao na wazazi na wadhamini mbalimbali
ambao wamekuwa nguzo kubwa ya kufanikisha mambo kadhaa ya maendeleo ya
mchezo wa kuogelea.
“Tuliweza kufanya semina kwa
makocha na waogeleaji wetu chini ya mkufunzi wa kimataifa na muogeleaji
nyota wa zamani wa Olimpiki, Penny Heyns wa Afrika Kusini. “Mafunzo
yalikuwa ya kisasa na sasa tunajivunia matunda yake, nawashukuru makocha
kwa kufanya kazi kubwa,” alisema.
Alisema kuwa makocha wao, Michael
Livingstone, Ferick Kalengela, Radhia Gereza, Kanisi Mabena, Adam
Kitururu, Simon Ngoya na Salum Mapunda wamekuwa nguzo kubwa ya kufikia
malengo yao.


0 comments :
Post a Comment