Mwenyekiti Wa Tume Ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) asema uchaguzi mwingine Z'bar hadi 2020.


Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha.
Sinema ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, ya kuishi kwa kujificha jana iliendelea, kutokana na kutokuonekana wakati wa kuingia na kutoka kwenye ukumbi wa kutangaza matokeo ya urais.
 
Viongozi mbalimbali wa serikali walionekana wakitoka kwenye magari yao na kuingia ukumbini na muda wa kutoka walionekana pia,  lakini Jecha alionekana akiwa amekaa meza kuu ukumbini bila kuonekana wakati wa kuingia wala kutoka.
 
Akizungumza na waangalizi wa uchaguzi, waandishi wa habari pamoja na viongozi wa serikali, Jecha aliwataka wanasiasa walioshiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika juzi kuwa wavumilivu na kuwataka waonane mwaka  2020.
 
Hata hivyo, hakufafanua kauli yake ya kuonana na wanasiasa mwaka 2020  kama bado atakuwa ni Mwenyekiti wa Zec ama ataonana nao akiwa mwananchi wa kawaida.
 
Jecha ambaye alionekana kuwa mtulivu na kutokuwa na maneno mengi, alizungumza kwa dakika 17 kwa kutoa maelezo ya awali kisha kumtangaza Dk. Ali Mohamed Shein  (CCM) kuwa mshindi wa urais wa Zanzibar.
 
Baada ya kuanza kuzungumza, wananchi mbalimbali waliokuwa ukumbini walilipuka kwa shangwe za kumshangilia, lakini ghafla walitulia.
 
Hata baada ya Dk. Shein kutangazwa mshindi na kukabidhiwa cheti, Jecha ambaye alikuwa mwenyeji wake, hakumsindikiza wakati wa kutoka, bali alitoka mwenyewe ukumbini na kusimama nje kisha kuhojiwa na waandishi wa habari.
 
Jecha hakuonekana nje hadi wageni wote waalikwa wanatawanyika katika eneo la Hoteli ya Bwawani yalipotangazwa matokeo hayo.
 
Kwa kipindi kirefu, Jecha amekuwa haonekani hadharani na mara ya mwisho wiki iliyopita alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa maandishi badala ya kuzungumza nao.
 
Muda wote kaunzia asubuhi eneo la Hoteli ya Bwawani kulikuwa na idadi kubwa ya askari wakiwa na siala za moto pamoja mbwa.
 
Magari yaliyokuwa yamebeba askari yaliingia eneo hilo na muda mfupi walinda amani hao walizunguka maeneo mbalimbali huku wakiwa na bunduki.
 
Watu wote walioingia walifuata utaratibu uliokuwa unaongozwa na askari, hali ambayo iliwafanya wananchi waliofika hapo kuwa watulivu kwa muda wote.
 
Akitoa shukrani baada ya kutangazwa mshindi, Dk. Shein alisema atahakikisha anatenda haki kwa wananchi wote wa Zanzibar.
 
Alisema matatizo ya kisiasa yaliyopo atahakikisha anayashughulikia ili Zanzibar iweze kupiga hatua za maendeleo.
 
Aliwashukuru Wazanzibari kwa kumchagua kwa kishindo na kuahidi kwamba jambo kubwa ni kuhakikishanchi inabaki kuwa tulivu.
Alimshukuru Rais John Magufuli kama Amiri Jeshi Mkuu kwa kudumisha amani na utulivu.
 
Aidha, alivishukuru vyombo vya dola kwa kufanya kazi ya ziada katika kipindi cha kuelekea uchaguzi hadi kutangazwa kwa matokeo.
SOURCE: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment