Dk. Ali Mohamed Shein.
Dk. Shein alitangazwa jana na Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha,
kuwa ameshinda uchaguzi huo uliofanyika juzi kwa kupata asilimia 91.4
ya kura zote kisha kumkabidhi cheti cha ushindi.
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi
Mkuu wa rais, wawakilishi na madiwani uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana,
kwa madai kuwa ulikuwa na kasoro kadhaa.
Msimamo wa kutomtambua Dk. Shein na serikali yake ulitolewa na
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alipokuwa
akizungumza na Nipashe kuhusu msimamo wa chama chake baada ya kufanyika
kwa uchaguzi huo.
Alisema kuwa uchaguzi huo ni batili na haramu kwa sababu uchaguzi
wa Zanzibar ulifanyika Oktoba 25, mwaka jana na ulikuwa huru na wa haki.
Alisema kuwa CUF kinajipanga kufanya tathmini juu ya hali ya
kisiasa Zanzibar na mwelekeo wake pamoja na kuangalia njia za kisiasa za
kukabiliana na CCM katika siasa za Zanzibar.
“Kitendo cha kutoshiriki uchaguzi kina maana kubwa sana kwa chama
cha CUF kwa sababu sasa tunafanya tathmini ya kuangalia hali ya kisiasa
ya Zanzibar na njia za kukabiliana na CCM katika siasa pamoja na
mustakibali wa Zanzibar,” alisema Shehe.
Alisema kwa mujibu wa ripoti za waangalizi wa ndani na nje wakiwamo
wa Jumuiya ya Ulaya (EU) na Jumuiya ya Madola, Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
25, mwaka jana ulikuwa huru na wa haki.
Alisema pamoja na kufanyika kwa uchaguzi wa Zanzibar, CUF
haitaitambua serikali wala kushirikiana nayo kutokana na upatikanaji
wake kuwa batili kupitia uchaguzi huo.
Aidha, alisema pamoja na waliokuwa wagombea wa CUF katika uchaguzi
wa mwaka jana kupigiwa kura licha ya kususia, kura hizo hawazitambui
pamoja na matokeo yake.
Alisema wagombea wote wa CUF akiwamo mgombea urais, Maalim Seif
Sharif Hamad na wagombea wa uwakilishi na udiwani walitangaza kujitoa
katika uchaguzi wa marudio na kwamba huo ndiyo msimamo Baraza Kuu la
Uongozi la chama hicho.
Hata hivyo, alisema kura walizopigiwa waliokuwa wagombea wa CUF
katika uchaguzi wa juzi ni mpango wa kutaka kuidaganya dunia kuwa CUF
ilishiriki katika uchaguzi wa marudio.
Alieleza kuwa CUF itaendelea kupigania haki ya wananchi iliyoporwa
na Jecha kwa kufuta matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana
kinyume cha matakwa ya Katiba na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.
Akizungumzia kukamatwa kwa viongozi wa CUF na kuendelea kubakia
mahabusu bila kupewa dhamana wala kufikishwa katika vyombo vya sheria,
mkurugenzi huyo alisema kitendo hicho ni kinyume cha misingi ya haki za
binadamu na utawala wa sheria.
Viongozi waliokamatwa kwa nyakati tofauti Machi 15 na Machi 18,
mwaka huu ni Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Hamad
Masoud Hamad na Mshauri wa mikakati wa KatibuMkuu wa CUF, Mansoor Yussuf
Himid.
Shehe alisema kitendo cha viongozi hao kuwekwa mahabusu na kunyimwa
haki ya dhamna ni uvunjaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala wa
sheria.
Alisema kwa mujibu wa wakili wao, viongozi hao wamekuwa
wakishikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mwembe Madema, Mkoa wa Mjini
Magharibi Unguja wakituhumiwa kwa makosa ya uchochezi na milipuko ya
mabomu.
SOURCE:
NIPASHE


0 comments :
Post a Comment