Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemfutia mashitaka ya kupokea rushwa ya Sh. milioni 161.7 za Tegeta Escrow, Mkurugenzi wa Fedha Benki Kuu Tanzania (BoT), Julius Angelo (49), baada ya upande wa Jamhuri kusema hauna nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Uamuzi huo ulielezwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, baada ya upande wa mashitaka kwa kutumia kifungu cha 98 (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kuiomba mahakama kuiondoa kesi hiyo.
Kwa upande wake, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Max Ally, alieleza kuwa, kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri jana.
“Mheshimiwa Hakimu, chini ya kifungu cha 98 (a) cha CPA, upande wa Jamhuri tunaona hatuna nia ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya mshtakiwa,” alieleza Max.
Hakimu Shahidi alisema kwa kuwa upande wa Jamhuri umeona hauna nia ya kuendelea na kesi hiyo, mahakama inaifuta na kumwachia huru mshtakiwa chini ya kifungu hicho.
Januari 16, 2015, kigogo huyo wa BoT, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, akikabiliwa na mashtaka ya kupokea rushwa.
Ilidaiwa kuwa, Februari 6, 2014 katika benki ya Mkombozi, jijini Dar es Salaam, alipokea Sh. milioni 161.7 kupitia akaunti namba 00120102646201.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alipokea fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Engineering and Marketing Ltd VIP, James Rugemalira, kama tuzo ya kusaidia kuidhinisha malipo kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kwenda PAP.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, mshtakiwa alifanya ishara ya msalaba na aliinamisha kichwa na kuibusu rozali aliyokuwa ameivaa.
Aidha, wanaodaiwa kuwa ndugu wa mshtakiwa huyo walitoka nje ya chumba cha mahakama hiyo huku wakifanya ishara ya msalaba, baadhi wakisikika wakisema: “Tunamshukuru sana Mungu… kweli Mungu ni mkubwa jamani,” huku wakiondoka katika eneo hilo la mahakama.
0 comments :
Post a Comment