Bundi ametua rasmi kwenye chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) cha CWT Tanzania wilaya ya Singida na kusababisha mkutano mkuu wa mwaka jana, kushindwa kufanyika kwa kile kilichodaiwa uongozi kushindwa kuwagawia wajumbe 234, kila moja kabrasha lake lenye  taarifa mbalimbali za mkutano huo nyeti.
Kitendo hicho cha uongozi kushindwa kuwapa wajumbe makabrasha yenye taarifa ya utendaji na ya mapato na matumizi ya mwaka jana, kilidaiwa ni uzembe uliopitiliza na hivyo,uongozi huo ukaagizwa kuwalipa posho kutoka mifukoni mwao (kila mjumbe shilingi 30,000), wajumbe wote waliohudhuria.
Aidha, baadhi ya wanachama wa SACCOS hiyo ambao hawakutaka majina yao yatajwe humu wamemwomba Mkuu wa wilaya ya Singida, aingilie kati kwa madai kuna jipu la kutisha ndani ya SACCOS hiyo.
IMG_3931
Mwenyekiti wa Chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) cha CWT Tanzania wilaya ya Singida, Selemani Sala akifungua mkutano wa wanachama wa CWT.
Baada ya Mwenyekiti wa SACCOS hiyo, Selemani Sala kufungua mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Singida, Andrew Msafiri,aliagiza taarifa ya utendaji na ya  mapato na matumizi ya mwaka jana, isomwe.
Agizo hilo lilizua vurugu kubwa baada ya wanachama kudai taarifa hiyo isisomwe hadi hapo muhtasari wa mkutano mkuu uliopita utakaposomwa na kupitishwa na pia kila mjumbe atakapopatiwa kabrasha lenye taarifa nzima ya utendaji kwa mwaka jana.
Kutokana na msimamo huo mkali kutoka kwa wananchama, Mwenyekiti Sala na Meneja wa SACCOS hiyo, Ezekiel Mashauri,walikaa pembeni na kuteta kwa muda juu ya namna bora ya kusafisha hali ya hewa iliyochafuka ndani ya mkutano huo.
Mwenyekiti Sala aliporejea kwenye kiti chake,alisimama na kusema kwamba kilichofanyika ni hujuma dhidi yake kwa madai kwamba siku moja kabla ya mkutano huo, waliweka kila kitu katika hali nzuri ikiwa ni pamoja na kila mwanachama kupatiwa kabrasha la taarifa.
“Kwa upande wangu sina dhambi kabisa,dhambi ipo kwenye nafasi ya meneja kwa sababu anazozijua  yeye  zilizopelekea ashindwe kuandaa makabrasha kwa ajili ya wajumbe wote kama ilivyo kawaida, na kupendekeza aondolewe”,alisema.
IMG_3925
Baada ya pendekezo hilo la Mwenyekiti, wanachama walipaza sauti na kusema “ondokeni wote”.
Kwa nyakati tofauti mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa Msafiri, Afisa Ushirika mkoa, Gurisha Msemo na Meneja uhusiano CRDB benki Singida mjini, Luhende Boaz,waliunga hoja za wanachama hao.
Hoja hizo ni pamoja na mkutano usifanyike, uongozi kutoka mifukoni mwao walipe posho za wajumbe waliohudhuria mkutano huo na gharama zingine za mkutano huo, na waitishe mkutano mwingine ndani ya mwezi moja kuanzia sasa.
SACCOS hiyo iliundwa kabla ya wilaya hiyo ya Singida haijagawanywa na kuwa wilaya mbili ikizaa wilaya ya Ikungi. Mkutano huo ulitarajiwa kugawanywa kwa SACCOS hiyo, ili kila wilaya iwe na SACCOS yake inayojitegemea.
Imeandaliwa na Na Nathaniel Limu