Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………………………………………………………
Na Felix Mwagara wa MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka
wananchi wa Zanzibar waondoe hofu kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu
visiwani humo.
Akizungumza mara baada ya kufanya mazungumzo na wananchi hao
wakati alipokuwa anatembelea mitaa mbalimbali ya Soko Kuu la mjini Chake
Chake, Pemba aliwataka wananchi hao waendelee na shughuli zao za
kujipatia kipato kama kawaida na hakuna mtu atakayewabughudhi kwani
ulinzi umeimarishwa, na waachane na uzushi wa kutokea vurugu unaoenezwa
visiwani humo.
Waziri Kitwanga alianza matembezi hayo mitaani mara baada ya
kufanya mazungumzo na Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Chake Chake
ambapo walimuhakikishia kuwa, Pemba yote ni salama na ulinzi
umeimarishwa na hakuna atakaye fanyiwa vurugu kwa mtu yeyote
atakayefuata sheria.
Waziri Kitwanga aliwataka wananchi hao kuondoa hofu wanapowaona
askari mbalimbali wakipita mitaani kwani wapo kwa ajili ya kuwalinda
wananchi hao pamoja na mali zao katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
“Musiwaogope askari, na wala msiwe na wasiwasi, mnapowaona
shangilieni kwani askari ndio msaada wako kwa ajili ya usalama wako
endapo inapotokea vurugu ya aina yoyote, mtaenda kupiga kura salama na
mtarudi salama, hakuna mtu wa kuwabughudhi, msitishwe na mtu yeyote,”
alisema Waziri Kitwanga na kufafanua;
“Leo nazunguka mitaa mbalimbali ya hapa Pemba, lengo ni kuchukua
maoni yenu pamoja na kuwaondolea hofu wananchi na kuwahakikishia vyombo
vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri kwa ajili ya kulinda
usalama, hivyo jitokezeni kwa wingi siku ya uchaguzi mkapigie kura
kiongozi mnaemtaka.”
Hata hivyo, Waziri Kitwanga alifanya ziara Mkoa wa Kaskazini
Pemba katika msitu wa Ngezi unaodaiwa kuwa kuna baadhi ya wakimbizi
wamejificha katika msitu huo ili kuokoa maisha yao baada ya kudaiwa kuwa
kutatokea na vurugu.
Kitwanga akiongozana na Wakuu wa Mikoa ya Kusini Pemba na
Kaskazini Pemba pamoja na maafisa wa Jeshi la Polisi Pemba, walienda
katika msitu huo na kuukagua na hawakukutana na mtu hata mmoja
aliyejificha msituni humo kama inavyodaiwa na kusambazwa habari na
baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar.
“Ndugu waandishi wa habari, tumezunguka kwa pamoja kuungalia
msitu huu, kuwatafuta hao wakimbizi, hatujamuona mtu yeyote, ukisikia
propaganda ndio hii, watu hawaitakii mema Zanzibar na Tanzania kiujumla,
mmeona kuwa habari hii ni ya uongo, hakuna mkimbizi yeyote katika msitu
huu kama tulivyoshuhudia wote kwa ujumla,” alisema Kiwanga.
Aliongeza kuwa, baadhi ya wananchi ambao wana mipango yao
binafsi wanawatia hofu wananchi kwa kutunga habari za uongo kuwa
Zanzibar imechafuka, wakati habari hizo hazina uhalisia wowote.
Hata hivyo, wananchi wa Pemba walimuhakikishia Waziri Kitwanga
wanafanya shughuli zao za kuwapatia kipato kama kawaida na pia siku ya
uchaguzi wataenda kupiga kura kama kawaida kwani wanaamini amani
itakuwepo kama ilivyokuwa sasa.
Waziri Kitwanga alifanya ziara Zanzibar katika Kisiwa cha Unguja
na kuzungumza na Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wakuu wa Vyombo vya
Ulinzi na Usalama, na baadae kumalizia ziara yake kwa kutembelea katika
mikoa yote ya Pemba ikiwa ni hatua ya kuangalia hali ya usalama visiwani
humo katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu katika maeneo hayo.


0 comments :
Post a Comment