Nkupamah media:
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi na watendaji wote wa Serikali
wahamie yalipo makao makuu ya wilaya ya Busega kuanzia sasa ili kuleta
kasi ya utendaji kazi kwenye wilaya hiyo ambayo ni mpya.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Machi 2, 2016) wakati akizungumza
na wananchi waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo
la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu. Waziri Mkuu
ambaye ameanza ziara ya siku sita ya mkoa huo atakagua shughuli za
maendeleo na kusalimia na wananchi katika wilaya zote za mkoa huo.
"Leo
nimeagiza watumishi wote wa umma katika wilaya hii wahame kutoka Magu
ambako wanaishi hivi sasa na wahamie hapa Busega ili wafanye kazi
kutokea hapahapa. najua kuna changamoto ya nyumba za watumishi lakini
waje waishi kwenye nyumba za kupanga wakati Serikali ikiendelea
kushawishi NHC, NSSF na Mwananchi Housing Corporation waje wajenge
nyumba za watumishi kwenye halmashauri mpya," alisema.
Waziri
Mkuu alisema kitendo cha watumishi kuhamia yalipo makao makuu ya wilaya
kitasaidia kuongeza kasi ya kuleta maendeleo kwani watakuwa wanaziona
changamoto zilizopo mahali wanapoishi. Alisema Serikali inao wajibu wa
kujenga ofisi na nyumba za watumishi na kuwahakikishia kuwa azma hiyo
itatimia kutokana na makusanyo ambayo Serikali imekuwa ikiyafanya hivi
sasa ikilinganisha na siku chache zilizopita.
Jengo
hilo la Halmashauri lililoanza kujengwa Julai 20, 2015 litagharimu sh.
bilioni 4.66/- na linatarajiwa kukamilika Januari 20, 2017.
Akisoma
taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya
Busega, Bibi Gaudensia Bamugileki alisema changamoto kubwa inayowakabili
ni kutopatiwa fedha kwa wakati hali ambayo alisema kama itaendelea
itaathiri ukamilishaji wa jengo hilo kwa wakati.
"Hadi
sasa mkandarasi ameshalipwa sh. milioni 600. Fedha ambazo zinahitajika
kukamilisha ujenzi ni sh. 4,064,580,238/-. Tunaendelea kukumbushia fedha
za ujenzi kutoka Serikali kuu ili tupunguze gharama ya kodi inayolipwa
kwa jengo la kukodi ambalo pia halitoshelezi mahitaji ya vyumba vya
ofisi kwa watendaji na watumishi wa Halmashauri," alisema.
Katika
mkutano mwingine, mara baada ya kukagua wodi ya akinamama, Waziri Mkuu
alizungumza na wakazi wa Nyashimo ambako wodi hiyo inajengwa na
kuwahakikishia nia ya Serikali kufikisha huduma bora kwa wananchi.
Alitoa
shukrani kwa ubalozi wa Japan kwa kuchangia ujenzi wa wodi kwa gharama
ya dola za marekani 80,000 pamoja na nyongeza ya sh. milioni 312.1. Pia
aliishukuru taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation ambayo tayari imejenga
nyumba 10 za watumishi kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Busega.
Pia
alisisitiza elimu kwa watoto wa kike na kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo,
Bw. Paul Mzindakaya afanye msako wa kubaini wale wote ambao hawajaanza
kidato cha kwanza hadi sasa. "Serikali inataka watoto wote waliofaulu
kwenda kidato cha kwanza wawe wameripoti shuleni. DC wewe ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hii. Fuatilia na kuwachukulia
hatua wote waaliozuia watoto hawa wasiende shule," alisema.
"Suala
la ulinzi kwa watoto wa kike hivi sasa ni la lazima. Ni lazima
tuhakikishe mtoto akianza shule ya awali anaingia darasa la kwanza
lazima amalize darasa la saba. Akiingia kidato cha kwanza, ni lazima
amalize kidato cha nne, akiingia kidato cha tano ni lazima amalize
kidato cha sita," alisisitiza huku akishangiliwa.
Mapema, akitoa
taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Simiyu, Bw. Elaston aliomba kuongezewa
ukomo wa bajeti ya mkoa kwa mwaka kwa sababu mkoa huo ni mpya na una
changamoto nyingi ikilinganishwa na mikoa ya zamani ambayo haina
mahitaji ya miundombinu.
"Mkoa
wa Simiyu umetengewa ukomo wa bajeti sh. 1,117,133,000.00 wakati mikoa
ya zamani kama Morogoro imetengewa sh. 2,836,225,000.00, Arusha
(2,595,571,000.00), Kilimanjaro (2,543,463,000.00) Mbeya
(2,141,239,000.00) na Tanga (2,318,545,000.00). Tunaomba tufikiriwa ili
tuweze kuimarisha miundombinu ya ofisi, barabara, na huduma za jamii
katika mkoa huu," alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 2, 2016.
0 comments :
Post a Comment