SIKU moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), George Simbachawene kutoa ushuhuda wa uzembe na unyanyasaji wa wagonjwa na waliofiwa katika Hospitali ya Sinza Palestina, Manispaa ya Ubungo, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, ameomba asaidiwe kufichua madudu zaidi.
Mganga huyo, Dk Mariam Maliwa alisema hayo jana alipotakiwa kuzungumzia kilio cha watu wengi kuhusu utendaji wa hospitali yake, akiwemo Waziri Simbachawene aliyelieleza gazeti hili kuwa, mkewe alishuhudia mwili wa kaka wa waziri huyo ukitupwa garini mithili ya mzoga, tena baada ya maneno mengi ya kejeli kwa wafiwa.
Alisema kwa sasa anaomba apewe muda ili aweze kufanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na Waziri Simbachawene. Aidha, alitaka kama kuna malalamiko mengine kutoka kwa wananchi waliohudumiwa katika hospitali hiyo na kukutana na shida mbalimbali, wafike hospitalini hapo ili wamuone wakiwa na maelezo kamili, siku na tarehe tukio husika lilipotokea ili aweze kuwasaidia, pia wasiwe na wasiwasi kwa kuwa hatawataja mahali popote.
“Wakati hayo yanazungumzwa na Waziri yanatokea, mimi nilikuwa Dodoma na sasa hivi nipo njiani ndio narudi, na mimi nimesikia hiyo stori nikiwa Dodoma, nipo njiani sijalifanyia kazi. “Naomba nilifanyie kazi hili la mheshimiwa kwanza.
Kama kuna wengine wana malalamiko yao nisaidie majina ya wahusika, tarehe za tukio na siku na sisi tunamlinda, hatutamtangaza au mhusika afike ofisini kwangu,” alisema Dk Maliwa.
Jana gazeti hili liliripoti kuwa Waziri Simbachawene ni miongoni mwa waathirika wa huduma mbaya na manyanyaso, wanayofanyiwa wagonjwa na hata wafiwa katika hospitali mbalimbali nchini.
Alisema hayo baada ya kufanyiwa unyanyasaji wa mwili wa marehemu kaka yake katika hospitali hiyo ya Sinza iliyopo wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam. Wakati Simbachawene akielezea hayo, mkazi wa jiji la Dar es Salaam ambaye hakutaka kutaja jina lake, ameelezea masikitiko yake kuhusu huduma mbovu za hospitali hiyo ya Sinza Palestina, ambazo anadai mtoto wake alifariki baada ya kunywa maji machafu, hali iliyochangiwa na uzembe wa watumishi waliokuwepo.
Aidha, alisema kabla ya mtoto wake kufariki alipata taarifa nyingine ya mtoto mwingine wa mke wa rafiki yake, ambaye inadaiwa alipokuwa anakaribia kujifungua aliomba msaada kwa watumishi waliokuwepo, lakini nao walimwambia bado muda, matokeo yake akiwa anashuka kitandani mtoto alidondoka na kupasuka kichwa kisha alifariki.
Mkazi huyo alisema kutokana na kitendo cha mtoto wake kufariki na mke wake kufanyiwa ukatili, kila anapokumbuka mpaka leo roho inamuuma kwa kuwa mke wake alipokuwa anakaribia kujifungua akiwa hospitalini hapo, aliomba msaada ambao hakuupata kwa haraka kutoka majira ya jioni hadi saa tisa usiku, alipopigiwa simu kuwa mke wake kajifungua.
Alisema asubuhi alikwenda na kukuta mkewe akiwa hana raha na alimweleza Mungu amemuepusha na kifo, kwa kuwa walitaka kumuua, wakati huo mtoto aliyezaliwa alikuwa chumba cha wagonjwa mahututi kwa kuwa alikunywa maji machafu.
“Baada ya kuwaendea viongozi na kuhoji kwa nini hali hiyo imetokea, mtoto wangu alipewa rufaa ya Mwananyamala ambako kule alikaa saa mbili tu kisha alifariki,” alisema. Alisema alipoomba ripoti ya mtoto wake kutoka Mwananyamala iliandikwa kuwa amekunywa maji machafu kwa uzembe, ripoti ambayo anayo mpaka leo.
0 comments :
Post a Comment