Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine (katikati) akimkabidhi
jezi ya Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Balozi wa StarTimes
barani Afrika Nwankwo Kanu kutoka nchini Nigeria, lengo ni kuthamini
mchango wake.Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania,
Lanfang Liao.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine, akizungumza na wadau
wa mpira nchini kwenye hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na
Kampuni ya StarTimes kwa lengo la kumkaribisha Balozi wa StarTimes
barani Afrika Nwankwo Kanu kutoka nchini Nigeria.
Balozi wa StarTimes barani Afrika
Nwankwo Kanu akizungumza na wadau wa mpira nchini kwenye hafla ya
chakula cha jioni kilichoandaliwa na Kampuni ya StarTimes kwa lengo la
kumkaribisha nchini mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine ameishukuru Kampuni ya
StarTimes Tanzania kwa kuthamini soka kwa kumleta nchini mchezaji nguli
wa kimataifa wa Nigeria, Nwanko Kanu.
Mwesiga aliyasema hayo mwishoni
mwa wiki jijini Dar es salaam kwenye hafla ya chakula cha jioni
kilichoandaliwa na Kampuni ya StarTimes kwa lengo la kumkaribisha Balozi
wa StarTimes barani Afrika Nwankwo Kanu kutoka nchini Nigeria.
“Kupitia StarTimes tutaboresha
mpira wetu kwa kuangalia ligi mbalimbali za mataifa ya Ujerumani, Italia
na Ufaransa” alisema Mwesigwa.
Ujio wa Kanu nchini ni fursa na
unamanufaa makubwa kwa mustakabali wa ukuaji wa soka hasa kwa kuzingatia
afya ya vijana katika michezo.
Kwa upande wake Balozi wa
StarTimes barani Afrika Nwankwo Kanu ambaye alikuwa mshambuliaji wa Timu
ya Taifa ya Nigeria (Super Eagles) amesema kuwa amekuja Tanzania kwa
mwaliko wa StarTimes na kuahidi kurudi kwa shughuli zake za kimichezo
maana amefurahishwa na mapokezi na anaamini mchango wake katika soka la
Tanzania unahitajika.
“Mustakabali wa mpira wa miguu wa
Tanzania utakuwa mkubwa kama Watanzania watapenda kufuatilia masuala ya
mpira wa miguu kupitia ligi tofauti tofauti, kadiri unavyoangalia
michezo mbalimbali ya kimataifa, ndivyo unavyozidi kujifunza” alisema
Kanu.
Kanu alifanyiwa upasuaji wa moyo
mwaka 1996 na ndipo alipoamua kufungua taasisi yake ya moyo inayoitwa
“The Kanu Heart Foundation.”
Taasisi hiyo iliyoko nchini
Nigeria ambako ndiko alipozaliwa aliianzisha kwa madhumuni makubwa ya
kusaidia wagonjwa wenye matatizo ya moyo na ameahidi taasisi hiyo
kushirikiana na taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika masuala
mbalimbali ya kitabibu.
Kanu mbali na kuchezea timu yake
ya Taifa, pia aliwahi kuchezea vilabu vya Iwuanyanwu Nationale kati ya
mwaka 1992 hadi 1993, mwaka 1993 hadi 1996 alichezea AFC Ajax,
mwaka 1996 hadi 1999 alichezea Inter Milan, mwaka 1999 hadi 2004
aliichezea Arsenal, mwaka 2004 hadi 2006 alichezea West Bromwich Albion
na mwkaa 2006 hadi 2012 alichezea Portsmouth.


0 comments :
Post a Comment