Basi la kampuni ya Hood lenye namba za usajili T 477 AXV Scania likiendeshwa na dereva Maxwell Kindole (42) Mhehe, mkazi wa Modeko, Morogoro mjini limepata ajali na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi watano.
Basi hilo lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Arusha liligonga Pikipiki yenye namba za usajili T 399 CCP, Toyo iliyokuwa ikiendeshwa na Gebra Munishi (19) mkazi wa Kibosho, Umbwe akitokea Himo kwenda Moshi na kusababisha kifo chake hapo hapo.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, SACP Wilbroad Mutafungwa  katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari tarehe 5/9/2016.
Pia ameeleza kwamba chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa Pikipiki kuhamia ghafla upande wa kulia akitaka kuingia kituo cha mafuta bila kuchukua tahadhari, wakati basi la Hood lilikuwa limeanza ku-over take Pikipiki hiyo iliyokuwa mbele.
“Dereva wa Pikipiki alihama upande wa kulia akitaka kuingia kituo cha mafuta bila kuchukua tahadhari, wakati basi la Hood lilikuwa limeanza ku-over take Pikipiki hiyo,” alisema SACP Mutafungwa.
Aidha Kamanda Mutafungwa amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya KCMC, Moshi na amewataja majeruhi watano kwenye ajali hiyo Damian Mate (35) mkazi wa Karatu, Ndesamu Ndesoa Shoo (32) mkazi wa Mbeya, Meryekzedeck Mrema (51) mkazi wa Same, John Rogers Mwihava (7) mkazi wa Dar es Salaam na Furaha Jumapili (18) mkazi wa Mbeya Mlowo wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi.