Bodi
ya Jukwa la Wahariri Tanzania (TEF) iliyokaa Ijumaa Aprili 22, 2016
jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine ilijadili hali ya mwenendo
wa tasnia ya habari nchini hasa juu ya haki ya wananchi kupata habari.
Katika
kujadili hali hiyo, TEF imeguswa kwa namna ya kipekee kabisa na
mwenendo mzima wa urushaji wa bahari za Bunge kwa njia ya redio na
luninga, hususan katika mkutano wa tatu wa Bunge la 11 unaoendelea mjini
Dodoma kwa sasa.
Itakumbukwa
kwamba Muhimili wa Bunge kupitia Kitengo chake cha Habari, Elimu na
Mawasiliano, Aprili 15 2016 ulitoa taarifa kwa umma ikieleza utaratibu
mpya ambao sasa umeanza kutumika katika kurusha matangazo ya redio na
luninga kutoka Bungeni.
Katika
taarifa hiyo, Ofisi ya Bunge ilisema kuwa imeamua kuboresha mfumo wa
urushaji wa Matangazo ya Bunge kwa Bunge lenyewe kurusha Matangazo ya
Vikao vyake pamoja na Vipindi mbalimbali vyenye Maudhui kuhusu Shughuli
za Bunge ambazo hazijapata fursa ya kufahamika vyema kwa umma kuanzia
katika Mkutano wa Bunge la Bajeti unaoendelea sasa.
Ofisi
hiyo ilisema kuwa mfumo huo mpya ni Utamaduni wa kawaida kwa kila Bunge
hususani Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola kuwa na Studio
zake kwa lengo la kurusha Matangazo ili yawafikie wadau kwa lengo la
kurusha kupitia vituo vyao.
Kwa maana hiyo, Bunge lilisisitiza kuwa chini ya utaratibu huo mpya,
jukumu la kurusha Matangzo ya Vikao vya Bunge litafanywa na Bunge
lenyewe kupitia FEED MAALUM ili kurahisisha kila Kituo cha Radio na
Televisheni kupata Matangazo hayo kwa sehemu walipo bila kufunga Mitambo
yao Bungeni Dodoma.
Katika
kutekeleza uamuzi huo na mfumo huo mpya, kila kituo cha Televisheni na
Redio sasa watatumia Masafa ya Matangazo ya Bunge (Frequencies) bure
kupitia FEED MAALUM itakayorushwa na Satellite ya INTELSAT 17 ambayo iko
nyuzi 66 Mashariki kwa masafa maalum ambayo pia yaliwekwa wazi.
Kwa
mantiki hiyo, Bunge sasa limezuia vituo vyote vya televisheni nchini
kupeleka kamera zake ndani ya Bunge kwa kuwa habari hizo zitapatikana
kwenye feed maalum ambayo ni ya Bunge ambayo inasimamiwa na waandishi wa
Bunge ambao pia ndio wanaamua nini kionyeshwe kwa utashi wao.
Baada ya kutafakari hatua hizi mpya za Bunge na baada ya kufuatilia kile kinachorushwa, mambo kadhaa yamethibitika:-
Mosi, habari kutoka ndani ya Bunge sasa zinachujwa mno kupitia mfumo huu mpya wa feed maalum;
Pili, ubora za picha zinazorushwa kupitia feed hii nao ni wa kiwango cha chini pia;
Tatu,
kwa mantiki ya kawaida kabisa, hatua hizi zote zimepunguza na kukwaza
haki ya wanahabari kufanya kazi yao kwa uhuru, lakini pia inawanyima
wananchi haki ya kupata kwa uhakika na bila kuchujwa kile kinachofanywa
na wawakilishi wao.
Kwa kuzingatia haya yote, TEF inasema bayana kwamba:
- Hatua hizi mpya za kuzuia kamera za televisheni kuingia Bungeni ni hatua za dhahiri kabisa za kukwaza uhuru wa habari nchini na kukuza censorship nchini. Hali hii haisaidii siyo Bunge tu, bali hata wabunge, wananchi na taifa kwa ujumla katika kupiga hatua za kweli katika kujenga demokrasia na kulinda haki za kupata habari na uhuru wa kujieleza nchini;
- TEF imeanza kuingiwa na hofu kwamba sababu za awali zilizokuwa zimetolewa za kuzuia utangazaji wa moja kwa moja wa Bunge kupitia TBC kwa sababu ya gharama, huenda hazikuwa za dhati. Hali hii imejionyesha hasa baada ya vituo binafsi vya televisheni kujitokeza na kuendelea kuonyesha vikao vya bunge moja moja, lakini navyo sasa vimenyimwa fursa hiyo kwa utaratibu huu mpya wa feed maalum.
- Ni dhahiri sasa, ushiriki wa wananchi katika kufuatilia mwenendo wa Bunge na wabunge wao umekwazwa sana kwa hatua hizi mpya na kwa maana hiyo, kupunguza ushiriki wa wananchi katika mfumo wa utawala wa nchi yao.
Kwa
kuzingatia haya yote, TEF inatoa rai kwa uongozi wa Bunge kufikiria
upya hatua hizi za kuzidi kufunika shughuli za Bunge kwenye blanketi
zito la usiri na censorship, hivyo uruhusu kituo chochote cha
televisheni chenye nia, uwezo na utayari wa kurusha matangazo ya Bunge
moja moja bila kulazimika kujiunga na feed maalum iliyoanzishwa.
Tunaamini
kwamba kama hali hii ya kutumia feed maalum itaachwa iendelee hakika
Tanzania kama taifa tunapiga hatua nyuma kwa yale mazuri machache
tuliyokuwa tumeyafikia, mojawapo, uhuru wa Bunge kuendesha mambo yake
kwa uhuru na uwazi mkubwa hivyo kuwa mfano mojawapo wa taasisi za umma
zinazojiendesha kwa uwazi.
Imetolewa leo, Jumapili Aprili 24 2016 jijijni Dar es Salaam na Jukwaa la Wahariri Tanzania.
Theophil Makunga Neville Meena
Mwenyekiti Katibu


0 comments :
Post a Comment