Kwa kutambua mchango wa wajasiliamali katika maendeleo ya nchi, Taasisi ya CITI iliyo chini ya benki ya Citi, imeandaa shindano litakalowahusisha wajasiriamali wadogo wadogo kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao watapata nafasi ya kushiriki na kushirikisha washiriki katika vipengele mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Uhusiano wa benki ya Citi, Frank Kallaghe, amesema thumuni la kuandaa shindano hilo ni kuangalia jinsi gani benki hiyo itaweza kuwatambua wajasiriamali nchini na hivyo wakaamua kuandaa shindano hilo ambalo mbali na washindi kupewa pesa pia watapatiwa tuzo na vyeti.
Amesema shindano hilo ni mara ya kwanza kufanyika nchini na litahusisha wajasiliamali ambao kupitia biashara wanazofanya kumeleta mabadiliko katika maisha yao, familia, jamii na pia biashara ambayo imeweza kutoa nafasi ya ajiraa kwa wengine.
“Tuliamua kuanzisha tuzo hizi baada ya kuangalia jinsi gani tutawatambua wajasiliamali wa Tanzania na katika tuzo hizo tunataraji kushirikisha wajasiliamali ambao biashara yao ipo tofauti kwa kuwasaidia kupata maendeleo,” amesema Kallaghe.
Afisa Uhusiano wa benki ya Citi, Frank Kallaghe akizungumzia shindano hilo.
Aidha Kallaghe ameongeza kuwa kwa kufanikisha shindano hilo kikamilifu wameshirikiana na Mtandao wa Asasi zinazotoa Huduma za Kifedha kwa Wajasiliamali Wadogo Wadogo TAMFI ili waweze kuwasaidia kuwatafuta wajasiliamali walio na vigezo vya kushiriki shindano hilo ambalo linatarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka huu.
Nae Katibu Mtendaji wa TAMFI, Winnie Terry amesema mbali ya kuangalia jinsi biashara imebadilisha maisha ya mshiriki pia anatakiwa awe amekopa katika taasisi ambazo zinatoa mikopo ya kifedha na jinsi gani anautumia mkopo huo ili kuzidi kuikuza biashara yake.
Bi. Terry ameongeza kuwa wanataraji kuendesha shindano hilo kwa kutumia majaji, maofisa wa Wizara ya Fedha na watu kutoka Taasisi mbalimbali za wajasiliamali ili kuhakikisha wanapata mshindi aliye na sifa za kutosha.
“Tutakuwa na watu ambao watakuwa wakipita kwa kila mjasiriamali kuona anafanya vipi biashara na kuangalia biashara hiyo imeboresha vipi maisha yake,” amesema Bi. Terry.
Katibu Mtendaji wa TAMFI, Winnie Terry akizungumzia jinsi washindi watapatikana.
Amesema shindano hilo litahusisha washiriki kutoka Dar es Salaam na Pwani na mbali na shindano la mjasiliamali bora pia kutakuwa na shindano la mjasiliamali mwanamke, mjasiliamali kijana na mjasiliamali mlemavu.
“Mshindi wa kwanza atapata Dola 7,500 (Mil. 15), mshindi wa pili Dola 6,000 ( Mil. 12), watatu Dola 4,000 (Mil. 8), mshindi wa shindano mama, kijana na walemavu kila mmoja atapata Dola 2,000 (Tsh. Mil. 4), wajasiliamali 10 kila mmoja Dola 1,000 (Mil. 2), Taasisi ya wajasiliamali Dola 2,500 (Mil. 5) na Afisa Mkopo ambaye anamsimamia mshindi wa mjasiliamali bora atapata Dola 1,500 (Mil. 3) ambapo kwa ujumla itatumika Dola 37,500 (Mil. 70),” amesema Bi. Terry.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Citi, Joseph Carasso amesema kuwa waliamua kuanzisha Taasisi ya CITI ili kuweza kusaidia jamii katika mambo mbalimbali na kupitia shindano hilo wataweza kuwasaidia wajasiriamali mbalimbali nchini ili waweze kukuza biashara zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Citi, Joseph Carasso akizungumzia Taasisi ya CITI na shindano hilo.
0 comments :
Post a Comment