Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa wafanyabiashara wa
vifaa vya mawasiliano, kuacha kuwahadaa wananchi kwa kutoa punguzo ili
kuwashawishi kununua simu bandia na kutishia kuwafunga miaka 10 jela,
faini ya Sh30 milioni au vyote kwa pamoja watakaobainika.
Hatua
hiyo imekuja wakati mamlaka hiyo ikiwa katika hatua ya kutekeleza mfumo
wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi,
huku ikitarajia kuzima simu feki ifikapo Juni 16.
Akizungumza
na vyombo vya habari jana Aprili 29.2016, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
TCRA, Mhandisi James Kiraba alisema kuna wafanyabiashara wajanja
wanaobadilisha namba za utambulisho za vifaa vya elektroniki (IMEI) ili
kuwahadaa wateja kuwa simu zao siyo feki.
Kwa ujanja huo, namba ya utambulisho inakuwa inatumika na simu zaidi ya moja na kutambulika na mfumo licha ya kuwa ni feki.
Pamoja
na kuonekana ni halisi kwa kipindi wanachozinunua, alisema simu hizo
zinazobadilishwa IMEI nazo zitazimwa Juni 16 kwa kuwa ni feki.
“Mamlaka
inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi kuwa ni kosa
kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mikononi (mobile
devices), kwani adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka 10 au faini
isiyopungua Sh30 milioni au vyote kwa pamoja,”alisema.
Alisema
kumekuwa na udanganyifu kwa baadhi ya wauzaji wa simu kwa kutoa punguzo
kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei nafuu.
Kiraba
alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na hilo, huku wakihakikisha kuwa
simu zao zimehakikiwa ili kuzuia usumbufu wa aina yoyote, utakaoweza
kujitokeza wakati kipindi cha mpito kitakapomalizika.
Alisema
idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia)
zimeendelea kupungua kutoka asilimia 30 Desemba mwaka jana hadi kufikia
asilimia 13 Machi.
Alisema
uchambuzi wa Februari ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo
zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia tatu, vilevile idadi
ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 18
huku simu halisi zilikuwa sawa na asilimia 79.
“Uchambuzi
wa Machi unaonyesha idadi ya namba tambulishi ambazo hazina viwango
zilikuwa sawa na asilimia nne, huku idadi ya namba tambulishi ambazo
zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 13, uchambuzi huu unahusisha
makampuni yote ya simu nchini,” alisema.


0 comments :
Post a Comment