Timu ya Taifa ya Burkina Faso imekuwa mshindi wa tatu wa mashindano ya
Afcon yanayoendelea nchini Gabon, baada ya kuifunga Ghana 1-0 katika
Uwanja wa Port-Gentil.
Mkwaju wa adhabu ndogo uliopigwa na Alain Traore katika dakika ya 89
uliomshinda kipa wa Black Stars, Richard Ofori ulitinga kimiani na
kuifanya Burkina Faso kutwaa nafasi hiyo, ambayo Ghana imekuwa
ikiitawala kwa muda mrefu.
Ghana ilitolewa na Cameroon katika hatua ya nusu fainali baada ya
kukubali kipigo cha 2-0, huku Burkina Faso ikiondoshwa na Mafarao wa
Misri kwa njia ya mikwaju ya penalti.
Leo usiku macho na masikio yataelekezwa Gabon kushuhudia fainali ya
kukata na shoka baina ya miamba ya Cameroon na Misri, mechi ambayo
itaamua bingwa wa mashindano hayo makubwa zaidi barani Afrika.
Misri ni mabingwa wa kihistoria wa Afcon kwa kuwa wametwaa taji hilo
mara saba, huku Cameroon maarufu kama Indomitable Lions wakitwaa ubingwa
huo mara nne.
0 comments :
Post a Comment