Washtakiwa wa Tumbili 61 Wanyimwa Dhamana



Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi imetupilia mbali maombi ya dhamana ya washtakiwa saba wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na wenzake sita, wakiwamo raia wawili wa Uholanzi.

Dk Mulokozi na wenzake walikamatwa Machi 23, mwaka huu wakitaka kusafirisha tumbili wekundu 61 kwenda nchini Armenia. Wanyama hao walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). 

Akitoa uamuzi huo juzi, Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Aishiel Sumari ambaye anasikiliza shauri hilo namba 1/2016, alisema mahakama hiyo imepima kwa umakini maombi ya dhamana dhidi ya washtakiwa hao na imeona hayana msingi, kwa kuwa suala lililopo mahakamani linagusa masilahi mapana ya Taifa. 

Jaji Sumari alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza maombi ya dhamana yaliyofunguliwa na mawakili wa utetezi, Majura Magafu, John Masangwa, Robert Rogath, Elibariki Maeda na Edward Silvester wakati Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na mawakili, Wankyo Simon na Salim Msemo. 
Wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Ofisa Mfawidhi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Kanda ya Kaskazini (Cites), Nyangabo Musika, Martina Nyakangara, VeryGerald Anthony (wote wakiwa ni maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii), Iddy Misanya anayedaiwa kukamata tumbili hao na Artem Verdanian na Eduard Verdanian ambao ni raia wa Uholanzi. 

Kutupiliwa mbali kwa maombi hayo ya dhamana kunafuatia uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga dhamana ya washtakiwa hao baada ya kuwasilisha mahakamani hati ya mwaka huu baada ya upelelezi kutokamilika, huku mahakama ikitoa kibali kwa mshtakiwa namba 6 kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi kutokana na kusumbuliwa na mgongo. 

Kunyimwa dhamana kwa watuhumiwa hao kumekuja wakati kukiwa na sintofahamu ya mtuhumiwa wa kesi ya utoroshaji nje ya nchi wanyamapori hai 136 wa aina 14 tofauti, wakiwamo twiga, Kamran Ahmed (29) aliyekuwa nje kwa dhamana, kutoweka nchini mwaka 2011. 
Mtuhumiwa huyo alitoweka siku chache baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi kumpa dhamana na kumtaka kusalimisha hati ya kusafiria. 

Awali, kabla ya kutoweka Ahmed alipewa dhamana yenye masharti ya kutosafiri nje ya Mkoa ya Kilimanjaro. 
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani mara ya kwanza katika Makahama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro, Juni 11, mwaka huo kwa tuhuma za kusafirisha na kutorosha nje ya nchi wanyamapori hao waliokuwa na thamani ya Sh170,572,000. 
Ahmed na wenzake walisomewa mashtaka sita tofauti, ikiwamo uhujumu uchumi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment