Meneja
wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Katavi Eng. Abdon
Maregesi akimuonesha athari za mvua Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia kwake) wakati akikagua daraja
la Koga lililoathirika. Daraja hilo linaunganisha mkoa wa Katavi na
Tabora.
Muonekano
wa Daraja la Koga baada ya kufanyiwa ukarabati kufuatia kuathiriwa na
mvua kubwa zilizonyesha katika mkoa wa Katavi. Daraja hilo kwa sasa
linaruhusu magari kupita ya tani 1 hadi 3.
Muonekano
wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa Km 356 inayojengwa kwa
kiwango cha lami ikiwa katika hatua za awali za ujenzi wake.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa mkandarasi wa kampuni ya CICO anayejenga barabara ya
Tabora-Koga- Mpanda yenye urefu wa Km 356, sehemu ya Tabora-Sikonge
kumaliza mradi huo kwa wakati.
Mkuu
wa Wilaya ya Sikonge Bi. Hanifa Sirengu akitoa taarifa kwa Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu hali ya
miundombinu katika wilaya yake.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
wakati alipotembelea kiwanja cha ndege cha Tabora.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisikiliza
maelezo ya namna vifaa vya kuongozea ndege vinavyofanya kazi kutoka kwa
mtaalamu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), mkoa wa Tabora.
Mkuu
wa Kikosi cha Zimamoto Uwanja wa ndege wa Tabora Bw. Yahya Nassoro
akitoa maelezo ya namna gari la kuzimia moto linavyofanya kazi katika
uwanja huo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema
Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza mradi wa ujenzi wa barabara
ya Tabora-Koga-Mpanda yenye urefu wa Km. 356 kwa kiwango cha lami ikiwa
ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano aliyoitoa kwa wananchi
wa Mikoa ya Katavi na Tabora.
Ametoa
kauli hiyo wilayani Sikonge mkoani Tabora, mara baada ya kukagua
barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amesema ujenzi huo
unatarajia kuanza rasmi hivi karibuni.
‘Ujenzi
wa barabara hii tumeugawa katika sehemu tatu ili kuharakisha
utekelezaji wake, tutahakikisha ifikapo mwisho wa mwaka huu, makandarasi
wote watatu watakuwa katika maeneo yao ya kazi’, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza
kuwa wananchi wanaostahili kulipwa fidia watalipwa kwa wakati kwa kuwa
takribani shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Prof.
Mbarawa pia amekagua daraja la Koga linalounganisha Mkoa wa Katavi na
Tabora na kuwataka viongozi wa mikoa hiyo kuhakikisha kuwa magari
yasiyozidi tani tatu ndio yanayopita katika daraja hilo ili kuepusha
ajali hadi ukarabati mkubwa utakapofanyika.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Kanali Mstaafu Issa Nziku amemuomba Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupandisha hadhi baadhi ya barabara
katika Wilaya hiyo ili zihudumiwe na Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), kutokana na uwezo mdogo wa Halmashauri hiyo kuzikarabati
kila wakati.
Katika
Hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua uwanja wa Ndege wa Tabora na
kuwataka viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mamlaka ya
Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) kuangalia namna bora ya ukarabati wa
kiwanja hicho ili uruhusu ndege kubwa kutua na kuongeza biashara.
Prof.
Mbarawa yuko katika ziara ya siku saba ya kukagua miundombinu ya
taasisi zilizo chini ya Wizara yake katika mikoa ya Magharibi ili
kuifungua kanda hiyo kimiundombinu na hivyo kufufua fursa za kiuchumi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 comments :
Post a Comment