Habari
zilizopatikana dakika chache mchana huu ni kuwa baadhi ya Madiwani wa
Jimbo la Misungwi pamoja na Wakereketwa wa jimbo hilo akiwemo Bw. Baraka
Kingamkono, Gaudency Tungaraza na Iddy Majumuisho kupitia kwa kampuni
ya CZ Information &Media Consultant Ltd imetoa taarifa za kumtetea
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa
Misungwi, Charles Kitwanga aliyevuliwa nafasi hiyo na Rais Dk. John
Pombe Magufuli kwa kile kilichoelezwa kuwa alijibu swali akiwa amelewa
pombe.
Taatifa
hiyo akisoma mbele ya waandishi wa Habari mbalimbali katika moja ya
ukumbi uliopo katikati ya Jiji, Cyprian Musiba kwa niaba ya Madiwani hao
huku akikataa kuulizwa maswali kwani yeye amepewa kazi moja tu ya
kuwasemea Madiwani hao.
Hata
hivyo, awali mkutano huo ulitakiwa kuongelewa katika Ukumbi wa Idara
Habari MAELEZO lakini haikuwezekana ndipo walipoamua kwenda kufanyia
katika ukumbi mwingine jirani na ukumbi huo wa Serikali kwa kile
kilichopatikana kuwa suala hilo lisinde kuwa ‘fear’ kwa Serikali kwa
chombo cha Serikali kutumika kutolea malalamiko ya kuilamu Serikali ama
Idara zilizo chini ya Serikali.
Soma hapa Taarifa hiyo ya Madiwani, Tazama tukio MO tv hapa chini:
UTANGULIZI
Ndugu
Waandishi wa habari, Karibuni kwenye mkutano huu mfupi ambao lengo lake
ni kutoa taarifa yetu fupi kuhusu ukweli uliojificha kuhusu kitendo
kilichopelekea Mh. Rais Dk. John Pombe Magufuli kutengua uteuzi wa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
Tunaamini kwa uwezo mliona kama waandishi wa habari, taarifa hii itafikia umma wa Watanzania kama ilivyokusudiwa.
UFAFANUZI
Kama
mnakumbuka mnamo tarehe 20 Mei mwaka huu, Rais Dk John Pombe Magufuli
alichukuwa uamuzi wa kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Misungwi kwa kosa la kwamba
Mhe. Kitwanga aliingia bungeni akiwa amelewa.
Sisi
wananchi wa Jimbo la Misungwi tumesikitishwa sana na taarifa na uamuzi
huu kwa kuwa tunaamini kuwa kuna dhamira iliyojifika iliyopelekea Mhe
Rais kufanya maamuzi haya. Ukweli ni kwamba huu ulikuwa mpango wenye
dhamira ovu na uliogubikwa na uongo mwingi ukilenga kumchonganisha
Mbunge wetu na Mhe. Raisi uliopangwa na waovu wachache ambao wamebanwa
na Serikali hii ya Awamu ya tano kupitia wizara hiyo nyeti kwa usalama
wa nchi.
Itakumbukwa
kuwa, Mhe Charles kitwanga alinadiwa na Mhe Rais na wanaCCM na baadae
kupigiwa kura kwa wingi na wananchi wa Misungwi kwa ajili ya uwezo wake
na dhamira yake njema ya kulinda taifa letu. Sisi wananchi wake,
tunaamini katika uwexo wake, uadilifu wake na nidhamu ya kazi aliyonayo,
hatuna mashaka na hili.
Baada
ya kuteuliwa na Mhe Raisi kama Waziri wa mambo ya ndani, amekuwa
muadilifu na kafanya mengi katika kuimarisha usalama na kufanya maamuzi
yengi mazuri kwa maslahi ya taifa. Hili lilimtengenezea maadui wengi
ndani ya serikali, ndani na nje ya CCM, mtandao wa dawa za kulevya,
walioachishwa kazi NIDA na Uhamiaji. Watu hawa ndio waliochochea na
kutengeneza mkakati wa kumchafua Mhe Kitwanga na walikuja dodoma
kuhakikisha dhamira yao ovu inatimia.
USHAHIDI WETU
Miongoni
mwetu tulikuwa mjini Dodoma pamoja na madiwani wa Jimbo la Misungwi
ambao tulikwenda kumtembelea Mbunge wetu bungeni, tulizungumza mengi kwa
ajli ya jimbo letu na katika kikao chetu hapakuwa na chembe ya kilevi
chochote na hata kesho yake alipoinga bungeni alikuwa mzima wa afya ya
kimwili na akili timamu na tunawahakikishieni kuwa Kitwanga hakuwa
amelewa.
Ndugu
waandishi wa habari asubuhi ya tarehe 20 tulielekea bungeni kwa mwaliko
wa Charles Kitwanga, tukiwa sehemu ya mualiko uliowajumuisha Madiwani
wa jimbo lake tukiwa tumeambatana naye tukaingia ndani ya ukumbi wa
bunge,tukashuhudia anajibu swali,baada ya kujibu swali la mbunge
Sakaya,tulitoka nje na kupiga picha na madiwani wote wa Misungwi
waliokuja kumtembelea Dodoma.
Baada
ya zoezi la kupiga picha kukamilika pale nje ya ukumbi wa Bunge,
tulitoka na kuelekea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la
kututembeza maeneo yote ya Dodoma , lakini ilipofika jioni wakati
tukirejea nyumbani tukiwa naye, ghafla tukaona habari zikisambazwa
kwenye mitandao ya kijamii kuwa Waziri Kitwanga amevuliwa uongozi kwa
kuwa alionekana na Waziri Mkuu akiwa amelewa.
Ndugu
wanahabari , tulishangazwa wote kwani tulikuwa tumekaa naye pale
nyumbani kwake Dodoma (site 2) tukipata chakula cha usiku ,alionekana
kutoaamini na hata madiwani pia na wengine ambao tulikuwepo hapa
nyumbani kwake hatukuamini.
Tunachosema
ni kwamba waziri Kitwanga hakulewa kama ambavyo imepotoshwa, bali
alikuwa ni mkakati wa kumchafua na kuhakikisha andavuliwa wadhifa wake
ili watu hawa waendelee kufanya maovu yao. Mtandao wa dawa za kulevya,
pamoja na wale waliokuwa wanamshutumu kwamba amehusika kuondolewa kwao
kazini wakiwemo Watu wa NIDA, Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani
Kikwete, Mfanyabiashara Said Lugumi pamoja na kundi mafisadi
waliokwapua mabilioni ya fedha NSSF. Pia na baadhi ya wabunge wa CCM na
Upinzani ambao walikuwa hawafurahishwi na kasi ya utendaji kazi wa
Kitwanga katika Wizara ya Mambo ya ndani.
Kwa
niaba ya wananchi wenzetu tunamuomba na kumtahadharisha Mhe. Rais awe
makini na makundi la wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, pamoja na
lile kundi la wanamtandao masalia ndani ya CCM na serikalini na kwenye
vyombo nyeti vya ulinzi na usalama, ambayo kwa ujumla yalikuwa na
mkakati kabambe wa kuhakikisha wanamtenganisha na kumpotosha Mhe Raisin a
kumjaza habari zisizo za kweli.
Ndugu
waandishi wa habari, kilichotushangaza zaidi baada tu ya Kitwanga
kuvuliwa madaraka yake ya uwaziri, kuna watu walianza kufanya sherehe
wakishangilia hususani wale waliovuliwa madaraka NIDA pamoja na
NSSF,Uhamiaji na wale wanaotuhumiwa kuhusika na madawa ya kulevya.
Ndugu
waandishi wa habari, tunajua namna kundi la Said Lugumi, Ridhiwani
Kikwete na kampuni yao walivyokuwa wanadhamini kwa mbinu za kifedha
katika vita hii ya kitwanga ili aondolewe, lakini baada ya kuondolewa,
wakajifanya kutoa taarifa ya kushangazwa kuondolewa kwake,
Kitwanga
amekuwa mtumishi wa serikali akiwa mtumishi mwandamizi benki kuu
Tanzania (BOT),amekuwa mbunge na Naibu waziri kwa miaka 10,lakini hata
siku moja hakuwahi kuonekana amelewa. Ni muadilifu na ana nidhamu ya
kazi, na nidhamu hii ndiyo iliyomfanya aaminiwe na kupewa dhamana hii.
MAAZIMIO YETU
=Tunaliomba
Bunge kumuomba radhi Mhe. Charles Kitwanga kwa kumdharirisha mbele ya
wapiga kura wake wa Jimbo la Misungwi familia yake pamoja na watanzania
wote waliokuwa wanaamini utendaji wake kupitia video iliyochezewa na
wataalamu wa IT katika studio za Bunge ili kufanikisha lengo la
kumuonyesha Kitwanga kuwa alikuwa amelewa bungeni.
=Tunamuomba
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ndiye Kiongozi Mkuu wa Serikali
bungeni atoe uthibitisho wa kikemia unaotanabaisha wazi kama Kitwanga
alikuwa katumia kilevi wakati akiwa bungeni maana hakuna kipimo chochote
kilichofanyika kudhibitisha uvumi huu.
=Tunaliomba
Bunge lifanye uchunguzi na kubaini wale wote walisambaza ile video
inayoonyesha Kitwanga akiwa anaongea na kuonekana amelewa wakati
kiuhalisia hakulewa na alijibu maswali yote vizuri
=Tunaliomba
Bunge kuchunguza idara ya habari ya Bunge pamoja na studio ile ya Bunge
ambao wamehusika na kuhariri ile picha ya video iliyokuwa inasambazwa
kwenye mitandao ya kijamii.
=Tunahoji
uhalali wa kumvua mtu madaraka kwa sababu ya ulevi bila uthibitisho wa
daktari ambaye kisheria ndiye mwenye mamlaka hayo kugundua kilevi cha
mtu.
=
Tunaomba Watanzania wote waliosikitishwa na taarifa hizi wajue tu kwamba
ile video ambayo imemtia hatiani Kitwanga ilihaririwa kwa ustadi mkubwa
kupitia wafanyakazi wa Bunge ambao wanapitia zile asadi za bunge pamoja
na baadhi ya wafanyakazi wa serikali kwenye vyombo vya ulinzi na
usalama ambao hawakupenda kitwanga aendelee kuwa pale ,kwa nia ya
kumhujumu na sasa wanasema kwenye vyombo vya habari ili kuhalalisha
uhujumu huo.
=Tunaomba
mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kuangalia picha zinazosambazwa
kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Mhe Mbunge wa Misungwi ambazo
zinaonekana kumchafua wachukue hatua dhidi ya watu hao kwani kisiasa
zinaendelea kumchafua na kumharibia kwa wapigakura wake,familia
yake,mama yake mzazi ,ndugu zake .
=Tunajiandaa
kuchukua hatua kwa Bunge za kisheria kama watashindwa kuthibitisha
tuhuma hizo dhidi ya Charles Kitwanga ambazo tunaamini zimetengenezwa
kwa maslahi ya makundi yanayompinga ndani ya Serikali wakiwemo mtandao
wa dawa za kulevya.
Pia
tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa makini kundi la
wanamtandao walio ndani ya serikali ambalo linaongozwa wahafidhina
wasio taka mabadiliko ndani ya serikali .
Imeandaliwa na madiwani wa Jimbo la Misungwi pamoja na wakereketwa wa jimbo hilo.
Baraka Kingamkono,Gaudency Tungaraza na IDDY Majumuisho.
Asanteni na Mungu awabariki.
Blogger Comment
Facebook Comment