Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma imeagizwa kufanya utafiti wa kina utakaowezesha kuwa na uwiano sawa wa malipo ya mishahara na masilahi ya watumishi wote serikalini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amesema hayo leo wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mkuchika amesema kuna baadhi ya taasisi/Idara za Serikali zinalipa watumishi wake mishahara mikubwa tofauti na taasisi nyingine jambo ambalo limekuwa likisababisha watumishi kutotulia sehemu moja na kutafuta masilahi bora zaidi sehemu nyingine.
“Hii haiwezekani, mmesoma darasa moja, fani moja na mko cheo kimoja, lakini mnalipwa mishahara tofauti wakati serikali ni moja, ni lazima mlifanyie utafiti wa kina suala hili. Masilahi ya watumishi wa umma lazima yawe sawa” Waziri
Mkuchika amesisitiza na kuongeza kuwa kumekuwa na malalamiko mengi serikalini kuhusu tofauti kubwa ya mishahara miongoni mwa watumishi wa Serikali Kuu na baadhi ya taasisi za serikali.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewataka watumishi wa Bodi hiyo kuwa wabunifu na kupendekeza mambo ambayo yatawavutia Watumishi wa Umma kufanya kazi Serikalini kwa dhati kwa kuzingatia taaluma zao na mgawanyo wa majukumu. “ Kila mtumishi ana taaluma yake na mgawanyo wa majukumu aliyopewa wakati anaanza kazi, hivyo ni vema kila mtu akazingatia hayo ili kuwa na utendaji bora serikalini,” Mhe. Mkuchika amesema.
Mhe. Mkuchika, ameendelea na ziara ya kikazi ya kujitambulisha na kujifunza kazi mbalimbali zinazofanywa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake, ambapo leo ametembelea Wakala ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA), Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma ni matokeo ya Tume ya Rais ya Malipo ya Mishahara ya mwaka 2006 iliyopewa jukumu la kuishauri Serikali namna ya kuboresha malipo ya mishahara na motisha nyingine katika Utumishi wa