Majina ambayo mashabiki wa Manchester United wamekuwa wakimuita Zlatan Ibrahimovic tangu alipowasili klabuni hapo yanaonekana kuanza kumponza baada ya mkongwe wa klabu hiyo, Eric Cantona kutoa maneno ambayo yanaonekana kumtahadharisha Ibra kuhusu heshima anayopewa na mashabiki.
Mashabiki wa Man United wamekuwa wakimuita Ibrahimovic, mfalme lakini Cantona amemwambia kuwa kumeshawahi kuwa na mfalme mmoja tu katika klabu hiyo na kama akitaka kupata nafasi basi atakuwa mtoto wa mfalme “Prince”.
“Nina ujumbe binafsi kwa Zlatan, umechagua kwenda Man United, ni uamuzi sahihi ambao umeufanya,” Cantona alisema wakati akifanya mahojiano na Eurosport na kuongeza.
“Jambo moja ni kuwa kuna mfalme mmoja Manchester. Unaweza kuwa mtoto wa mfalme kama ukihitaji na jezi namba 7 ni yako kama ukihitaji. Hii ndiyo zawadi yangu ya ukaribisho kwako. Mfalme ameshaondoka, nakutakia mafanikio mema mtoto wa mfalme”