![]() |
JAJI
Paulo Kihwelo aliyesikiliza kesi ya mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Daudi Mwangosi ameteuliwa na Rais John
Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Jaji
Kihwelo atakayetoa hukumu ya kesi hiyo Julai 21, mwaka huu anachukua nafasi
iliyoachwa wazi na Jaji Ferdinand Wambali aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Taarifa kutoka Ofisi ya Jaji Mkuu Dar es
Salaam kwa vyombo vya habari, ilisema kabla ya uteuzi huo Jaji Kihwelo alikuwa
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa taarifa, Jaji Kihwelo pia
aliwahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria kati ya mwaka 2009 na 2010, katika Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na aliwahi pia kushika nafasi ya Mkurugenzi wa
Kurugenzi ya Kudhibiti Viwango na Ubora.
Taarifa hiyo ilisema Jaji Kihwelo alipata
Shahada ya Uzamivu ya Sheria (PhD) katika Chuo Kikuu Huria mwaka 2009, Shahada
ya Uzamili ya Sheria (LL.M) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka
2000 na Shahada ya kwanza ya Sheria (LL.B) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
mwaka 1997.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
kilianzishwa mwaka 1998 na kilianza kutoa mafunzo mwaka 2000.
Chuo kinatoa mafunzo ya Stashahada ya
Sheria na Cheti au Astashahada ya Sheria, ambapo kina jumla ya wanafunzi 514
wanaoendelea na masomo kwa ngazi hizo. Kadhalika chuo kinatoa mafunzo endelevu
kazini kwa majaji, mahakimu na maofisa wa mahakama.



Blogger Comment
Facebook Comment