Askofu wa kanisa la Pentekoste (FPCT) tawi la Singida mjini,Dk.Paulo Samwel,amewaasa waumini na wananchi kwa ujumla, kujiepusha na tabia ya kukopa mikopo wasiyo na uwezo wa kuirejesha kwa wakati.
Amedai tabia ya kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati,inasababisha usumbufu mkubwa ikiwemo kukimbia mji bila kupenda.
Askofu Dk.Samwel ametoa tahadhari hiyo wakati akitoa nasaha zake kwenye ibada maalum ya kufunga kongamano la wiki moja lililohudhuriwa na wanawake waumini wa kanisa hilo.
Alisema uzoefu unaonyesha wazi kuwa waumini na watu wengine wenye tabia ya kukopa ovyo ovyo,maisha yao hutawaliwa na hofu na wasi wasi mkubwa wakati wote.
“Mimi na mwenzangu mchungaji Boniface, kwa kifupi tumechoshwa na malalamiko mengi yanayohusu mikopo isiyolipika.Waumini wenzangu hasa wale wanaokopa ovyo,wakati mnakopeshana mnakuwa wawili …..mkopaji na mkopeshaji.Mkopaji akishindwa kurejesha mkopo mnaanza kukimbilia kwa watu.Hapana,acheni kusumbua watu malizeni wenyewe,” alifafanua Dk.Samwel.
Akisisitiza, alisema kuwa ni bora muumini au mwananchi yoyote alale na njaa, kuliko kukimbilia kukopa wakati uwezo wa kurejesha mkopo hana.
“Ndugu zangu mikopo ina madhara mengi tena mengine ni makubwa zaidi.Wapo baadhi ya wakopaji hukatisha maisha yao kutokana na mkopo,wapo wanaofikia uamuzi wa kujificha chini ya uvungu wa kitanda wakiogopa kudaiwa.Ukimuuliza mwanafamilia fulani yupo wapi,atakijibiwa kasafiri kumbe yupo kwenye uvungu wa kitanda,” amefafanua zaidi.
Aidha, askofu Dk.Samwel alisema wapo baadhi ya waumini au wasiowaumini, wakimwona mtu amejaliwa kiuchumi,wanaanzisha urafiki wa kinafiki.
“Shida yao ni waweze kukopa ovyo.Kabla hujaenda kukopa,jikague kwanza kama una uwezo wa kurejesha mkopo husika kwa wakati.Kama huna acha kabisa kukopa ili uendelee kuishi kwa amani na utulivu,na heshima yako iendelee kuimarika,” alisema askofu huyo.
Wakati huo huo,askofu Dk,Paulo,amewataka waumini wenye madeni yakiwemo ya taasisi za kifedha zinazotoa mikopo,kulipa madene hayo mapema ili waendelee kuishi kwa ustaarabu na kuheshimika mbele ya macho ya jamii.
Na Nathaniel Limu