Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameitaka serikali ya Ethiopia kutoa fursa kwa waangalizi huru kutembelea maeneo ya Oromia na Amhara kufuatia tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu ambao umeripotiwa kufanywa na vyombo vya usalama katika maeneo hayo.
Mbali na kueleza wasiwasi alionao kufuatia ripoti kwamba ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulifanywa katika maeneo ya Oromia na Amhara katika maandamano ya kupinga serikali yaliyofanywa katika kipindi cha tarehe 6 hadi 8 mwezi huu, Al Hussein ameitaka serikali ya Addis Ababa ifungue milango kwa ajili ya mageuzi ya kisiasa na kidemokrasia.
Zeid Ra'ad Al  Hussein
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein.
Amesisitizia serikali ya Ethiopia kuwaruhusu haraka iwezekanavyo wataalamu wa masuala ya haki za binadamu kutembelea maeneo yenye mzozo ili kutathmini hali ya mambo.
Ravina Shamdasani, msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema wanakaribisha uamuzi wa kuanzisha uchunguzi huru na wanaihimiza serikali ya Ethiopia ihakikishe uchunguzi huo unakuwa na mamlaka ya kufuatilia madai ya ukiukaji wa haki za binadamu tangu machafuko yalipoanza katika eneo la Oromia mwezi Novemba mwaka 2015.
Amesisitiza kuwa uchunguzi huo uwe huru, wa wazi, kamili na athirifu ili kuona kama zilitumika nguvu na kuhakikisha wahusika wa ukiukaji wowote wa haki za binadamu wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Kwa mujibu wa chama cha upinzani cha Oromo Fedarilist Congress watu wasiopungua 33 wameuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama vya nchi hiyo wakati wa maandamano ya kupinga serikali katika mkoa wa Oromia.
Na Regina Mkonde