Mwanamuziki wa miondoko ya Taarab pamoja na Miduara nchini Tanzania, Kassim Mganga, ameeleza kusikitishwa na Kundi la Tip Top kutokutoa nyimbo mpya kwa muda mrefu sasa na wakati wasanii bado wapo na wenye uwezo mkubwa wa kufanya kitu.
Akizungumza hayo katika kipindi cha Power Jams cha East Africa Radio, Mganga amesema kuwa tangu aondoke katika kundi hilo hajaona wakitoa vitu vya kutosha japo hajui ni nini wamekipanga kwa siku za karibuni kwenye ulimwengu wa burudani wenye changamoto nyingi sana.
“Unajua nimekuwa nje ya Kundi kwa muda sasa japo mimi bado ni mwanafamilia lakini siwezi jua ni kitu gani hasa kimesababisha wao kukaa kimya kwa kipindi chote hiki na swala hili linanigusa sana roho yangu wakiwa kama watu wenye vipaji vikubwa na uwezo wa kufanya jambo” alisema Kassim
Aidha aliongeza kuwa kwa sasa soko linahitaji ubunifu wa hali ya juu na kukaa kwake kwa muda mrefu kimya alikuwa akitaka watu wammiss wakumbuke kwamba kulikuwa na mtu na kama yeye na wakati huo huo akiwa anasuka kitu kingine kwa ajili ya mashabiki zake.
Mganga ambaye amezingua Audio ya nyimbo yake mpya aliyoipa jina Manuari amesema kuwa tangu alipotoa Subira watu walitegemea alete kitu kama kile kile cha kuchezeka kidogo lakini ameamua kuachia wimbo wa Taratibu wenye heshima na adabu kwa wapenzi na mashabiki wake wa muziki.
“Manuari ipo kidogo kama Subira ila huu ni wimbo wenye heshima na Adabu na hauna kuchezeka kama ulivyokuwa ule, nilichofanya ni kuzungumzia mapenzi na hasa ukitulia na mtu wako wa karibu ni wimbo mzuri sana katika mahusiano,” aliongeza Mganga.
Subira ni wimbo aliokuwa amemshirikisha msanii Christian Bella na ni moja kati ya nyimbo zilizowahi kumvusha mipaka ya Tanzania kutokana na uzuri wa nyimbo yenyewe huku mkali huyo akiwahi kutamba na nyimbo kama `I Love You`, `Awena`, pamoja na Tajiri wa Mahaba aliomshirikisha Mr. Blue nyimbo iliyotengenezwa na mtayarishaji muziki Bob Junior ndani ya Sharobaro Records.
Na Derick Highiness