Makundi mawili ya wanamgambo kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yameahidi kusaidia hatua za kurejesha amani nchini humo.
Muungano wa makundi yanayobeba silaha mashariki mwa Congo DRC uitwao “Umoja wa Wazalendo wa Kongo Huru na Inayojitawala” na kundi la wanamgambo wa Mai Mai yanayoendesha harakati zao katika maeneo ya kaskazaini mashariki mwa nchi yamesaini hati ya makubaliano na kuahidi kufanya jitihada za kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.
Makundi hayo pia yameahidi kuchukua hatua ili kukomesha mapigano, machafuko na kuondoa vizuizi vinavyokwamisha harakati za watu kuingia na kutoka kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano hayo ilifanyika jana katika mji wa Muganga, katika mkoa wenye machafuko wa Kivu Kaskazini chini ya usimamizi wa wabunge wa mkoa huo.
Hitilafu za kugombania umiliki wa vyanzo vya madini na ardhi na ushindani wa baadhi ya madola ya eneo, zinatajwa kuwa sababu kuu za mapigano na migogoro katika eneo hilo.
Kwa mwaka wa 20 sasa, maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa ni uwanja wa vita na mapigano makali yanayohusisha makundi kadhaa ya wanamgambo katika maeneo hayo.
Na Regina Mkonde
0 comments :
Post a Comment