UAMUZI wa Kambi ya Upinzani bungeni kuingia katika vikao vya Bunge na
kugeuka bubu wakati wa mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
umechukuliwa kwa hadhari kuwa unaweza kusababisha kambi hiyo ionekane
inalinda posho bungeni.
Hadhari hiyo imetolewa na wasomi na viongozi mbalimbali waliozungumza na
gazeti hili jana, walipokuwa wakitoa maoni kuhusu uamuzi wa kambi hiyo
kususa hotuba hiyo.
Dk Bana
Mhadhiri wa fani ya siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk Benson Bana, ndiye aliyesema kuwa kama uamuzi huo wa kuwa
bubu bungeni hautabadilishwa, kambi hiyo itaonekana inalinda posho na
kwamba haipo kwa ajili ya kutetea wananchi.
“Kazi yao ni kuwakilisha wananchi na makundi yote bungeni, sasa kitendo
cha kuota ububu na kushindwa kueleza kero za wananchi, ni kutotendea
haki wananchi maana ni vema wakae bungeni na kutoa hoja zao la sivyo,
itafika wakati watatuomba radhi wananchi,” alisisitiza.
Akizungumzia hoja ya kwanza ya Mwenyekiti wa kambi hiyo, Mbunge wa Hai,
Freeman Mbowe (Chadema), kulalamikia muundo wa Serikali kutowekwa
gazetini, Dk Bana alihoji kama Mbowe hajui kuwa muundo wa Serikali
hautolewi kwa kila mtu.
Kuhusu suala la fedha zilizokatwa katika Mfuko wa Bunge na kuelekezwa
katika utengenezaji wa madawati, Dk Bana aliwashangaa wawakilishi hao wa
wananchi wanaopingana na uamuzi wa kumuinua mwananchi wa kawaida.
Alisema wananchi wote walipendezwa na hatua hiyo ya Serikali ya kuchukua
fedha zilizotoka bungeni baada ya kubana matumizi na kupeleka katika
kununua madawati.
“Hatua hii ni kielelezo kuwa Bunge lilikuwa likipangiwa fedha nyingi
kuliko matumizi yake hivyo kusababisha kuwepo matumizi ya hovyo, sasa
viongozi wa Bunge kuliona hilo na kurejeshwa kwenye jamii ni jambo
jema,” alisema.
Alionya kuwa mikakati ya kambi ya upinzani, ni kutetea wananchi lakini
kwenye hilo wananchi wenyewe kila kona wanawashangaa kwani inaonesha
kutetea maslahi ya wabunge.
Bashiru Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally
alisema wananchi wanaangalia vitendo vya wabunge wao ndani ya Bunge na
watawahukumu kwani michango yao ndani ya Bunge ni muhimu na njia ya
kutatua tatizo si kususa, bali kufuata taratibu za kisheria.
Alisema uamuzi wa kutozungumza, unaondoa maana ya vyama vya upinzani
ndani ya Bunge kwa kuwa watashindwa kujadili masuala yenye manufaa ya
wananchi, kwani mawazo ya kiongozi wa upinzani bungeni ni muhimu na
yanawekwa kwenye kumbukumbu.
“Kuwekwa kwenye kumbukumbu mawazo hayo ni kwa ajili ya vizazi vijavyo,
sasa kitendo cha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kutumia vibaya
nafasi anayopewa, ni udhaifu wa kimkakati,” alisisitiza Bashiru.
Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema
wanavyofanya wapinzani ni jambo lisilopendeza katika kuleta umoja wa
kitaifa, kwani wao ni wawakilishi wa wananchi ndani ya Bunge na kususa
siyo jambo la kiungwana.
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment