Viongozi wa vyama vya siasa nchini wametakiwa kutotoa kauli zinazodaiwa kuwa za uchochezi kutokana kwamba kauli hizo zinaweza zikavunja umoja, ushirikiano na amani nchini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya Ukuta inayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka huu nchi nzima
“Ushauri wangu watu wa vyama vyote wafuate sheria, viongozi wa siasa waache kutoa kauli zitakazochochea uvunjifu wa amani na waheshimu mamlaka zenye uhalali kisheria pindi zinapotoa maamuzi,” amesema.
Amesema Septemba mosi kuna matukio mbalimbali yenye manufaa kwa taifa na kuwataka wananchi kutoshiriki katika maandamano hayo.
“Mbali na wanasiasa kutoa kauli za uchochezi zitakazosababisha kuvuruga amani, umoja na mshikamano, wananchi pia wasishiriki maandamano hayo yatakayosababisha uvunjifu wa amani,” amesema na kuongeza.
“Tarehe moja kuna matukio mengi yenye faida kwa taifa ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuadhimisha miaka 52 na kupatwa kwa jua ambapo inatarajiwa watalii wengi watakuja nchini, sasa kama wakisikia hali si shwari watakuja,tutapata mapato?”
“Tarehe moja kuna matukio mengi yenye faida kwa taifa ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuadhimisha miaka 52 na kupatwa kwa jua ambapo inatarajiwa watalii wengi watakuja nchini, sasa kama wakisikia hali si shwari watakuja,tutapata mapato?”
Masaju amesema kuwa ni vyema vyama vya siasa vikatumia njia za awali za kusuluhisha mvutano wa kisiasa uliopo ikiwa ni pamoja na kuketi katika kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kinachotarajiwa kufanyika Septemba 3 hadi 4 mwaka huu.
Aidha ametoa wito kwa viongozi wa dini kuliombea taifa amani na kusihi vyama vya siasa vilivyopanga kufanya maandamano kutofanya maandamano hayo.
“Naomba viongozi wa dini wafanye maombi dhidi ya hii hali ya baadhi ya watu kutoheshimu sheria pamoja na kuzuia maandamano hayo,” amesema.
Hivi karibuni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitangaza kufanya maandamano yasiyo ya kikomo nchi nzima yatakayofuata baada ya uzinduzi wa operesheni Ukuta Septemba 1, 2016.
Hata hivyo Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kilitangaza kufanya maandamano waliyodai kuwa ni ya kupongeza utendaji kazi wa Rais John Magufuli.
Na Regina Mkonde
0 comments :
Post a Comment