Taarifa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu –(MOI) mchana huu wa leo Agosti 26.2016 imeeleza kuwa, hali ya Bwana Jenerali Ulimwengu inaendelea vizuri na anaendelea na matibabu.
Akizungumza na Mtandao wa Nkupamah media, kwa njia ya simu, Afisa Uhusiano wa MOI, Bw. Patrick Mvungi, amesema kuwa Jenerali Ulimwengu alipelekwa hospitalini hapo mnamo majira ya saa kumi na moja alfajiri na anaendelea na matibabu chini ya wataalamu.
“Ni kweli yupo katika kitengo chetu na aliletwa mida ya saa Kumi na moja alfajiri. Kwa sasa anaendelea vizuri ikiwemo kupata huduma chini ya wataalamu wetu hapa kwa kuendelea kuhudumiwa na kupewa matibabu” alibainisha Afisa Habari huyo.
Awali Habari zilizopatikana zilieleza kuwa, Jeneraali Ulimwengu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Gazeti la Raia Mwema, amepata ajali na kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku ajali hiyo ikielezwa kuwa imehusisha gari alilokuwa akiendesha Jenerali mwenyewe aina ya Benz pamoja na gari niyngine iliyoigonga gari yake upande wa ubavuni.
Jenerali Ulimwengu ni nani?:
Jenereali ulimwengu alizaliwa mkoani kagera mwaka 1948 katika wilaya ya Ngara, elimu yake ya msingi aliipatia mkoa wa Bukoba na baada ya hapo alikwenda kujiunga na shule ya Sekondari Nyakato ambapo alimaliza kidato cha 4 mwaka 1966 na baada ya hapo alifaulu na kwenda kusoma elimu ya kidato cha sita ‘Tabora Boys’.
Mnamo Julai mwaka 1969 alikwenda jeshini kupata mafunzo ya uzalendo ‘National Service’ Mafinga na Nachingwea kwa muda wa miezi sitaq na baada ya hapo alikwenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sheria (LLB) ambayo alimaliza mwaka 1972.
Jenerali ni mwandishi nguli wa habari nchini Tanzania lakini hivi sasa ni mwenyekiti wa Bodi ya Gazeti la Raia Mwema
Na Hashim Ibrahim (UDSM-SJMC)
0 comments :
Post a Comment