Chama cha ACT-Wazalendo kimepanga kuitisha mkutano mkuu wa kidemokrasia wa ndani Septemba 24,2016. Lengo la mkutano huo uliopewa jina la Kongamano la Kidemokrasia ni kujadili hali ya maendeleo na uelekeo wa nchi pamoja na masuala ya Bara la Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ACT Ado Shaibu amesema kongamano hilo la kidemokrasia litashirikisha wadau, wanachama, na wafadhili wa chama hicho pamoja na baadhi ya wananchi watakaojisajiri kushiriki katika kongamano hilo.
“ACT kimekusudia kuitisha mkutano mkuu wa kidemokrasia, hii ni haki yetu kikatiba na hata kwa dunia nzima si ajabu kwa kuwa vyama vya siasa hufanya hivyo. Kongamano hili litawaleta pamoja wanachama, wadau na wafadhili wa ACT ambao watajadili hali ya maendeleo ya nchi,” amesema na kuongeza.
“Hatutaja mahali na ukumbi tutakaoufanyia kwa sasa, wakati ukifika tutawajulisha.Na hatutaomba kibali kwa kuwa katiba haisemi vyama vya siasa kuomba kibali vinapotaka kufanya mikutano ya ndani.”
Shaibu amesema kuwa endapo serikali itazuia kufanyika kongamano hilo watachukua hatua za kisheria kupinga maamuzi hayo kwa madai kuwa katiba ya nchi na ya vyama vya siasa inarushusu kufanyika.
“Serikali ilituzia kufanya mikutano na vikao vya ndani, tulikaa kimya awali tukiamini kuwa tutaishawishi kwa hoja na itajirekebisa lakini haikufanya hivyo.Tunaamini serikali itarudi nyuma na kuamini haina mamlaka ya kuzuia mikutano na vikao vya ndani kwa sababu kuizuia inamaana unafuta shughuli za siasa na sisi tutakuwa wa mwisho kukubali vyama kufutwa ,” amesema.
Amesema ACT haitokuwa nyuma kuiunga mkono serikali inapofanya vyema na kwamba endapo chama hicho kitakosoa utendaji kazi wake, serikali isikichukie kwa kuwa kinatekeleza wajibu wajibu wake.
Kwa upande mwingine, Shaibu amesema Kamati Kuu ya Uongozi wa Chama cha ACT imefanya baadhi ya marekebisho ya muundo wa uendeshaji kwa kuteua baadhi ya makatibu wa kamati za chama hicho.
“Kikao cha tatu cha kamati kuu kilichoketi Septemba 5,2016 kilifanya teuzi mbalimbali za makatibu, sambamba na kugawa baadhi ya kamati ikiwemo iliyokuwa kamati ya Ulinzi, Usalama na Uadilifu ambapo kwa sasa imegawanyika na kuwa kamati ya Usalama na Ulinzi na mpya ni Kamati ya Uadilifu, ” amesema.
Amewataja makatibu wapya wa kamati walioteuliwa akiwemo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Chama cha Wananchi CUF (JUVICUF) Mohamed Babu ambaye kwa sasa ni Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Ally Kifu ameteuliwa kuwa Katibu wa kamati ya Fedha na Miradi ya Kujitegemea. Katibu mwengine aliyeteuliwa ni Sabrah Mohamed ambaye ameshikilia Kitengo cha Kushughulikia Maendeleo ya Zanzibar.