Dereva Mario Sabas Mgaya (22) mkazi wa Mlangali Ludewa, amehukumiwa na mahakama ya wilaya ya Singida adhabu ya kutumikia jela miaka mitatu jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujipatia shilingi 50 milioni kwa njia ya utapeli.
Aidha, mahakama hiyo imemwamuru kumrejeshea kiasi hicho cha shilingi 50 milioni ambazo zilikuwa ni mafao ya kustaafu mwalimu Welu Timothi Kitonka mkazi wa kiomboi wilaya ya Iramba. Alimtapeli kwa kumuuzia dhahabu ‘feki’.
Kiasi hicho cha fedha atazirejesha baada ya kumaliza adhabu ya kutumikia jela miaka mitatu.
Mwendesha mashitaka wakili wa serikali Michael Ngoboko alidai mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya ya Singida Flora Ndale, kuwa aprili 13, 2013 saa 2:30 asubuhi, huko katika maeneo ya NMB benki, mshatakiwa alijipatia shilingi 50 milioni mali ya mwalimu mstaafu Welu Timoth Kitonka, baada ya kuumuuzia dhahabu feki.
Akifafanua,Ngoboko alisema aprili 11, 2013, mwalimu mstaafu Welu alikabidhiwa hundi na halmashauri ya wilaya ya Iramba mafao ya kustaafu ya shilingi 53, 858, 711, 00.
Alisema mwalimu Welu baada ya kutoka ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Iramba alikuwa na hundi yake mkononi, alikutana na Ritha Mathias ambaye alimwomba amuonyeshe ofisi za Wachina wajenzi wa barabara.
“Baada ya kuambiwa Wachina waliIshahama, Ritha alimwambia mwalimu huyo mstaafu kuwa, wana madini ya thamani kubwa wanayoyauza. Akamshawishi anunue kwa madai atapata faida ya zaidi shilingi laki sita,” alisema.
Akifanunua zaidi, Ngoboko alisema Ritha alimwita Mario Sabasi Mgaya ambaye alifika eneo la tukio kwa taksi na kumuonyesha mwalimu mstaafu Welu dhahabu ‘feki’.
Alisema baada ya kushawishiwa mwalimu Welu aliwaambia watu hao matapeli kuwa yeye hana shilingi 50 milioni taslimu isipokuwa ana hundi ya mafao ya kustaafu yenye kiasi hicho cha fedha na zaidi.
“Baada ya kuonyesha hundi hiyo hundi hiyo ya shilingi 53,858,711,00, ndipo aliposhauriwa waje Singida mjini kutoa fedha hizo kwenye benki ya Nmb. Mwalimu Welu alikubaliana na ushauri huo na kuondoka kuja Singida mjini,” alisema Ngoboko.
Alisema walipofika Singida mjini, mwalimu Welu aliongozana na Ritha wakaingia Nmb na kuingiza hundi hiyo kwenye akaunti yake, na wakati huo huo akajaza fomu ya kutoa shilingi 50 milioni.
“Afisa wa Nmb banki Singida alimuoji mwalimu Welu juu ya lengo la kuchukua kiasi hicho kikubwa kwa mkupuo.Welu alimjibu afisa huyo wa benki kuwa anakwenda kununua nyumba ya Ritha ambaye aliambatana naye,” alisema.
Ngoboko alisema baada ya kujitetea hivyo alipewa kiasi hicho cha fedha na kisha walipotoka nje ya benki na kuingia kwenye taksi, alimkabidha mshatakiwa Mario Sebasi Mgaya, na yeye mwalimu akapewa dhahabu feki.
Alisema mwalimu Welu alipokwenda kwa mfanyabiashara wa madini, aliambiwa hiyo sio dhahabu ameliwa. Baada ya kuelezwa hivyo, alifika kituo cha polisi mjini hapa na kufungua kesi yaliyopelekea mshatakiwa Mario kukamatwa akiwa mjini Morogoro.
Akitoa hukumu hiyo hakimu Ndale alisema upande wa mshatakiwaumethibitisha bila kuacha shaka yo yote, kuwa mshatakiwa ana hatia kama alivyoshitakiwa.
“Mahakama hii inakuhukumu adhabu ya kutumikia jela miaka mitatu na ukimaliza adhabu yako, urejeshe shilingi 50 milioni za mwalimu mstaafu Welu,” alisema hakimu Ndale.