Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa siku 9 tangu
kutokea kwa tetemeko la ardhi katika maeneo mbalimbali ya nchi huku
athari kubwa ikionekana zaidi mkoani Kagera, serikali bado haijatoa
mwelekeo wenye kutia moyo na kuwapatia matumaini waathirika wa maafa
hayo makubwa.
CHADEMA kimesema kuwa wakati Serikali ikiwa inasuasua katika kasi ya kusaidia wananchi wa Kagera kukabili athari za janga hilo, muda unazidi kwenda huku maelfu ya watu waliokumbwa na maafa wakiendelea kukosa msaada wa uhakika wa kibinadamu kutoka serikalini.
CHADEMA kimeitaka Serikali kutimiza wajibu wake kwa waathirika hao ikiwa ni pamoja na rais kufika mkoani humo kuwafariji waathirika ambao wamefiwa, wamejeruhiwa na kupoteza mali na makazi.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Salum Mwalim Jumapili, Septemba 18, usiku alipokuwa akizungumza katika kikao kilichoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Wilfred Lwakatare kwa ajili ya kuwaelezea wenyeji wa Mkoa wa Kagera wanaoishi Dar es salaam kuhusu maafa ya tetemeko hilo na hali ilivyo hadi sasa.
Mwalim amesema kuwa ni vyema Serikali ikatambua wajibu wake na kuutimiza kwa haraka, badala ya kuendelea kusisitiza watu kuacha siasa katika jambo hilo.
Mwalim amesema inasikitisha kuona serikali ikisuasua katika jambo hilo licha ya kuelezewa kama mojawapo ya majanga kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini.
Amesema kuwa haikubaliki kwa serikali kutegemea misaada ya wahisani na taasisi binafsi pekee wakati Serikali ikiwa na mfuko wa maafa unaotengewa bajeti kila mwaka, ilitakiwa kuwa imeshatoa fedha kwenda kusaidia waathirika.
Kaimu Katibu Mkuy pia ameshangazwa na hatua ya Rais Dk. John Magufuli hadi sasa kutokwenda kutoa mkono wa pole kwa waathirika, ikiwa ni zaidi ya wiki moja tangu kutokea kwa tukio hilo.



0 comments :
Post a Comment