Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeahirisha mikutano na
maandamano ya hadhara ya UKUTA iliyopanga kuifanya kesho nchi nzima na
kwamba itatangaza siku na tarehe itakayopangwa baadae kwa kuzingatia
hali halisi ya kisiasa itakavyokuwa nchini.
Mwenyekiti
wa Chama hicho, Freeman Aikael Mbowe amesema kuwa sababu iliyopelekea
kuahirisha maandamano hayo kwa sasa, ni kuwa chama hicho kinapanga
kutumia mbinu za kidiplomasia pamoja na harakati nyingine ili
kufanikisha UKUTA pasipo kuathiri wanachama wake na nchi kiujumla.
“Siku
ya jana, Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya chama chetu ilikutana ili
kutafakari hali ya kisiasa nchini, kamati imetujulisha kuwa hadi leo
viongozi wa dini hawajatupa taarifa zozote kuhusu jitihada zao za
kuonana na rais Magufuli, kutokana na hilo, kamati hiyo imeona bora
isogeze siku na tarehe nyingine ambayo hatutaitaja kwa sababu taarifa
zetu za intelijensia zinaonyesha kuwa kila tukitaja tarehe wenzetu
wanapanga njama za kuua watu siku hiyo ili kuwaaminisha watu kuwa UKUTA
ndiyo imeua watu,” amesema.
Amesema
kufuatia jeshi la polisi kuondoa zuio la mikutano ya ndani, chama hicho
kitaitumia fursa hiyo kutekeleza UKUTA pamoja na kukijenga chama hicho.
“Kufuatia
kuondolewa kwa zuio haramu la mikutano ya ndani ya vyama vya siasa,
kamati maalumu ya Kamati Kuu imeamua kufanya ziara katika Kanda na mikoa
ya kichama ili kuendeleza harakati za UKUTA, kujenga na kuimarisha uhai
wa chama chetu na UKAWA,” amesema.
Ametaja
mbinu nyingine ya kutekeleza UKUTA kuwa ni kuishtaki serikali katika
jumuiya za kimataifa pamoja na taasisi zinazoshughulikia masuala ya haki
za binadamu duniani.
“Baadhi
ya viongozi wetu walifanya ziara nchi za nje ya nchi kuelezea mataifa
namna ya uvunjwaji wa haki unavyoendelea nchini, tutakwenda katika nchi
za Asia, Amerika, Umoja wa Afrika na taasisi zinazoshuhulika na masuala
ya haki za binadamu,” amesema.
Aidha,
Mbowe amesema kamati maalumu ya Kamati Kuu ya chama hicho, imeelezwa
juu ya maandalizi ya kufungua mashauri mahakamani kupinga hatua alizodai
kuwa ni za ukandamizaji wa demokrasia na haki za binadamu pamoja na
ukiukwaji wa katiba na sheria za nchi.


0 comments :
Post a Comment